NA TERESIA MHAGAMA,TANGA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.Doto Biteko ameeleza
kuwa Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan anataka kuona viongozi wote
wanatatua kero na changamoto za wananchi na kwamba anasikitishwa na
baadhi ya viongozi ambao hawatatui changamoto za wananchi mpaka pale
anapofanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini.
Dk.Biteko amesema hayo leo Januari 25, 2024 wakati akizungumza
na wananchi katika Kijiji cha Magodi na Kigandini wilayani Mkinga
mkoani Tanga mara baada ya kuwasha umeme katika vijiji hivyo ambao
umesambazwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Katika ziara yake kwenye Vijiji hivyo, aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa
Tanga, Waziri Kindamba, Mbunge wa Mkinga ambaye ni Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.
“Mhe. Rais anafanya kazi kubwa katika kila Sekta na mabilioni ya pesa
yamekuwa yakipelekwa kila Mkoa kwa ajili ya kuboresha huduma za
wananchi, nikitolea mfano hapa Tanga Serikali ya Awamu ya Sita
imeshaleta shilingi Trilioni 2 na Bilioni 600 kwa ajili ya miradi ya
maendeleo, kwenye umeme miradi inaongezeka kwani mmepata bilioni 133.6
huku Wilaya ya Mkinga ikipata bilioni Nane kwa ajili ya usambazaji
umeme, Dkt. Samia anapambana ili kuwaletea maisha bora watanzania
hivyo viongozi wengine tusiishie kusikiliza kero tu bali tuzitatue na
kama kuna mahali tunahitaji watupe muda, tuwaambie kwa uwazi.” amesema
Dk.Biteko
Katika hatua nyigine, Dk.Biteko amewataka Wazazi na Walezi nchini
kupeleka Shule watoto wote wanaostahili kuwa mashuleni katika kipindi
hiki ambacho Shule zimefunguliwa ili wapate elimu itakayowasaidia
katika maisha yao na nchi kwa ujumla, akitolea mfano kwa Mkoa wa Tanga
watoto walioripoti Shule ni asilimia 60.
Hivyo, ameagiza viongozi kusimamia suala hilo ikiwemo kuendesha msako
na kutumia sheria zilizopo kwa wale wanaoficha watoto ili wasiende
shule kwani ifikapo mwezi Machi watoto wote wanatakiwa wawe wameripoti
shuleni.
Kuhusu usambazaji umeme vijijini, amepongeza REA kwa kuendelea
kusambaza umeme vijijini akitolea mfano kuwa, usambazaji umeme
vijijini mkoani Tanga umefanyika kwa asilimia 91 na wilaya ya Mkinga
yenye Vijiji 85 tayari vijiji 82 vimesambaziwa umeme huku kazi ya
kusambaza umeme kwenye vijiji vilivyosalia ikiendelea na baadaye
vitafuata vitongoji.
Kuhusu hali ya umeme nchini, amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya
kila jitihada kuboresha hali hiyo kwa kuhakikisha kuwa mitambo ya
umeme inafanyiwa maboresho na miradi mipya inaanzishwa na kutekelezwa
akitolea mfano kituo cha umeme cha New Pangani (MW 68) kinatarajiwa
kuzalisha umeme baada ya siku mbili baada ya kufanyiwa maboresho.
Akiwa katika Kijiji cha Magodi, Dk. Biteko amechangia Sh.
Milioni 5 kwa ajili ya kusaidia kubadilisha paa la zahanati ya kijiji
hicho ambalo limechakaa na kuahidi kumalizia ujenzi wa jingo la
Madrasa katika Kijiji hicho.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mkinga ambaye ni Naibu Waziri wa Maliasili
na Utalii, Dunstan Kitandula ameishukuru Serikali kwa kutekeleza
kwa ubora miradi ya umeme vijijini wilayani humo na kuwafanya wananchi
kufanya shughuli za kiuchumi pamoja kuboresha utoaji wa huduma kwenye
maeneo mbalimbali kama vile vituo vya Afya na Shule.
Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kusambaza umeme kwenye maeneo
mengine yaliyosalia kama vile vitongojini ili wananchi katika maeneo
hayo pia wapate huduma ya umeme.