NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR
OFISI ya Rais, Mipango na Uwekezaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amekabidhi nyenzo za utendajikazi kwa Timu Kuu ya Wataalamu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikiwa ni nyaraka muhimu zitakazotumika katika sehemu ya uaandaaji wa Dira 2050.
Akizungumza leo Januari 13, 2024, Zanzibar wakati akifungua warsha elekezi ya Timu Kuu ya Wataalamu ya Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, Mhe. Prof. Mkumbo amesema
“Tunawakabidhi nyenzo muhimu za kufanyakazi ambazo ni nyaraka za masuala mbalimbali yaliyotokea kabla ya Uhuru, wakati wa Uhuru na baada ya Uhuru, Ripoti mbalimbali kuanzia mwaka 1961 hadi 1991, Ripoti ya Jaji Warioba na Dira ya mwaka 2025”.
Prof. Kitila ameendelea kutaja nyenzo zingine kuwa “Taarifa ya Tathimini ya Dira 2025, Muongozo wa Maandalizi ya Dira 2050, hotuba ya Mhe. Rais aliyoitoa katika Mkutano wa Kwanza wa Kitaifa wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hotuba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu Dira, maelezo yangu mimi kuhusu Dira 2050 niliyoyatoa katika Mkutano wa Kwanza wa Kitaifa wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na nyaraka nyingine muhimu, pia nitawakabidhi hadidu za rejea”.
Katika hatua nyingine, amesema kuwa Dira ya mwaka 2050 inatarajiwa kuwa jumuishi na shirikishi kwa lengo la kufanya Watanzania kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao ya namna nchi itakavyokuwa miaka ijayo.
“Dira ya mwaka 2050 izingatie ushiriki na ujumuishi, lazima Watanzania wafike mahali waseme hii ni Dira yetu, si ya Serikali hivyo lazima Watanzania washiriki.
Pia, ni lazima iwe ya kijamii, kitaaluma na kisiasa, kila kundi ni muhimu kushiriki”, ameeleza Prof. Mkumbo. Pia,
Ameitaka Timu Kuu ya Wataalamu ya Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kushiriki kikamilifu katika kazi hiyo, kuwa mstari wa mbele katika kuwasilisha mawazo mbalimbali Serikalini, kuwa na nafasi ya kujifunza kutoka katika maeneo na watu mbalimbali duniani kwa lengo la kuandaa Dira yenye kukidhi mahitaji kulingana na ukuaji wa teknolojia na mazingira ya sasa.
Naye, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida amesema kuwa kuanzia mwaka 2023 tayari kuna kazi ambazo zilishafanyika, mfano tayari muongozo wa maandalizi ya Dira ambao unaobainisha mchakato na jinsi ya kuifanya kazi hiyo, maeneo ya msingi yatakayozingatiwa kwenye Dira, mpango wa kazi, bajeti, nyaraka zinazobainisha uzoefu wa nchi nyingine katika Dira zao za Maendeleo.
“Hivyo katika zoezi hili la ukusanyaji maoni kuna kazi baadhi zimeshafanyika, ushauri wangu kwenye timu ni kuangalia nini kimefanyika, kitu gani tunaweza kukichukua katika yale yaliyofanyika, nini tunaweza kukiongeza na nini tunaweza kukiboresha katika kuandaa Dira 2050”, ameeleza Katibu Mkuu Dk. Kida.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru amesema kuwa Lengo la warsha hiyo ya Timu Kuu ya Wataalamu ya Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni kujenga uelewa wa pamoja kwa Timu ya Wataalam ya Uandishi wa Dira kuhusu mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Tunafanya hivi ili kila mmoja wetu aelewe majukumu atakayo kuwa nayo katika uandaaji wa Dira na kufahamu hatua zote muhimu katika uandishi wa Dira, 2050.
Vile vile kwa kuwa baadhi ya wajumbe katika timu hizi kitaaluma sio wanamipango na katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku hawajihusishi na shughuli za mipango ya maendeleo ni vyema tukapata fursa ya kukakaa pamoja na kubadilishana mawazo kabla ya kuanza rasmi kutekeleza majukumu yaliyo mbele yetu”, ameeleza Mafuru.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Dk. Rahma Salim Mahfoudh amesema “Katika kuandaa Dira hii, ni vyema kuhakikisha kwamba tunakuwa na ushirikishwaji wa kutosha, tuangalie ule ushiriki ambao ulishafanyika na kuboresha zaidi. Tuweke Dira ambayo itakuwa na uhalisia”.
Mwenyekiti wa Timu Kuu ya Wataalamu ya Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Prof. Lucian Msambichaka ameishukuru Serikali kwa kuiamini Timu hiyo kwa kuipa jukumu hilo muhimu kwa taifa na ameahidi kuwa Timu hiyo itafanyakazi kwa juhudi zaidi kwa kuwa Watanzania na dunia kwa jumla ina matarajio makubwa katika kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Ombi letu ni kupata ushirikiano katika ngazi mbalimbali za uongozi na makundi mbalimbali ya jamii.”
Pia Watanzania watoe ushirikiano ili tuweze kumaliza jukumu hili kwa muda uliopangwa na sisi tutafanyakazi nzuri kwa manufaa ya taifa.