- MWANAMKE ,mwanamke, wala siyo mwanamme,
Yeye ana mambo yake, mwache wala simseme,
Tena na akili yake, mwangalie mtazame,
Moyo wake mwanamke, si kama wa mwanamme. - Wanadamu wote sawa, hiyo yapigiwa shime,
Kuna mambo tuko sawa, twaweza tuyatazame,
Mengine ninayagawa, kila mtu ajipime,
Moyo wake mwanamke, si kama wa mwanamme. - Huruma ya mwanamke, si kama ya mwanamme,
Abaki na njaa yake, kwa mwingine ajitume,
Huo ndio moyo wake, si kama wa mwanaume,
Moyo wake mwanamke, si kama wa mwanamme. - Anaweza akajua, kwamba wewe mwanamme,
Ya wengine watatua, yeye wamwacha akome,
Yako atayatatua, hata watu wamseme,
Moyo wake mwanamke, si kama wa mwanamme. - Akipenda mwanamke, ampendaye ni ngome,
Kumwona aruke ruke, na kwingineko avume,
Siyo kawaida yake, hapa bora nimseme,
Moyo wake mwanamke, si kama wa mwanamme. - Hata kama asikia, uovu wa kwake mume,
Atazidi mfanyia, mema yule mwanamme,
Si sawa akasikia, huyo ndugu wa kiume,
Moyo wake mwanamke, si kama wa mwanamme. - Hata kwa mambo ya ndoa, wa kike si wa kiume,
Mke akaa kwa ndoa, atakavyo mwanamme,
Na wa pili akioa, mke akaa kwa mume,
Moyo wake mwanamke, si kama wa mwanamme. - Ndiyo tuna wake wenza, kwa mmoja mwanamme,
Nadra waume wenza, mke mmoja aseme,
Hili jambo latufunza, mke si sawa na mume,
Moyo wake mwanamke, si kama wa mwanamme. - Amani ya duniani, mwanamke siyo mume,
Furaha ya duniani, mwanamke siyo mume,
Shida nyingi duniani, sababu ya wanaume,
Moyo wake mwanamke, si kama wa mwanamme. - Wanawake wanajua, michepuko ya waume,
Hatua za kuchukua, si kama za wanaume,
Wanaishi wakijua, machafu yao waume,
Moyo wake mwanamke, si kama wa mwanamme. - Mwanamme akijua mke anacho kidume,
Achukuazo hatua, vurugu nzima zivume,
Hata yule tunajua, anachepuka kiume,
Moyo wake mwanamke, si kama wa mwananme. - Tuwatunze vema hawa, na tusiwaseme seme,
Wasije wakachachawa, wang’ake sisi tukome,
Heshima wakipatiwa, watatuenzi waume,
Moyo wake mwanamke, si kama wa mwananme.
Na Lwaga Mwambande
lwagha@gmail.com 0767223602