- TUNATEKWA hatujui,
Tunategwa hatujui,
Tunashikwa hatujui,
Akili ituingie. - Utandawazi ni chui,
Makucha ni buibui,
Chochote hatuambui,
Akili ituingie. - Kama tumechanjwa ndui,
Ugonjwa hautuui,
Hadhari hatuchukui,
Akili ituingie. - Kama vile hatukui,
Anavyokuja adui,
Kama hatumtambui,
Akili ituingie. - Runinga hatuchagui?
Vishikwambi siyo tui?
Simujanja hatujui?
Akili ituingie. - Kaenda huko adui,
Ajua hatutambui,
Twaona hatuugui,
Akili ituingie. - Kamari hatuijui?
Kwani hiyo si adui?
Mkwanja hatuchagui,
Akili ituingie. - Ufundi hatufungui,
Na shida hatutatui,
Mkeka hatuujui?
Akili ituingie. - Vyakula hatuchagui,
Twaugua hatujui,
Chochote hatubagui,
Akili ituingie. - Hekima hatuangui,
Chini hatuzifukui,
Zaja hatuzichukui,
Akili ituingie. - Kwani sisi hatujui,
Na kazi hawachagui,
Wapate hawatanui,
Akili ituingie. - Mbona samaki huvui,
Hizo nyavu huchukui,
Kubeti hakupungui?
Akili ituingie. - Kwani watu hawaui,
Mapicha hawatanui,
Bunduki hawachukui?
Akili ituingie. - App hatuzipakui?
Na muda hazichukui?
Twaona hatuugui?
Akili ituingie. - Kwani picha hatujui,
Wala sisi hatukui,
Waigiza hatujui?
Akili ituingie. - Muda wenda hatujui,
Matunda hatutungui,
Mtego hatutegui,
Akili ituingie. - Vitabu hatuvijui,
Mapya hatuyazibui,
Wala hatujisumbui,
Akili ituingie. - Vichekesho hatujui,
Ya kwetu havitatui,
Tunacheka hatukui,
Akili ituingie. - Kama miti haikui,
Matunda hatuchungui,
Tunajua hatujui,
Akili ituingie. - Milango hatufungui,
Na vyumba hatuchagui,
Twararua kama chui,
Akili ituingie. - Pengine hatuugui,
Mirembe hatuijui,
Ila ndiyo hatukui,
Akili ituingie. - Tuyafanye yenye tui,
Na kuvaa baibui,
Ndani mtu hachungui,
Akili ituingie. - Joto halituchubui,
Hata tuwe chuichui,
Kwao sisi hatujui,
Akili ituingie.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602