*Yahimiza wenye sarafu kwenda kuzibadilisha kupata noti
*Huduma kutolewa kwenye Benki za biashara
NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
IMEELEZWA kuwa uanzishwaji Mfumo Mpya wa Utekelezaji Sera ya Fedha kwa kutumia Riba ya Benki Kuu( Central Bank Interest rate) unafuta ujazi wa fedha.
Ikumbukwe kwamba, mfumo uliokuwa ukitumika awali ulifikia kikomo mwishoni kwa mwaka jana ambapo ulidumu kwa miaka 28.
Aidha hivi karibuni BoT itatangaza kwa mara ya kwanza kiwango cha riba chini ya utaratibu huo mpya uliofanyiwa mabadiliko
Hayo yameelezwa leo Januari 9,2024 na Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi, BoT, Dk. Suleiman Missango alipozungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuhusu Mfumo Mpya wa Uandaaji wa Sera ya Fedha (Interest Rate-Based Monetary Policy Framework) na Ukusanyaji wa Sarafu.
Dk Missango amebainisha kuwa, Utekelezaji wa Mfumo wa Riba ya Benki Kuu umeonesha matokeo mazuri katika usimamizi wa sera ya fedha na kuimarisha misingi ya utekelezaji wake katika mazingira ya uwazi katika nchi mbalimbali duniani na kutoa mfano wa , Afrika Kusini, Mauritius,Ghana na kwa Afrika Mashariki nchi ya kwanza kutumia mfumo huo ametaja kuwa ni Uganda.
Aidha duniani ,nchi ya kwanza ilikuwa New Zealand, iliyofuatiwa na Uingereza mwaka 1990.
Sababu nyingine alisisitiza, mfumo huo wa kutumia riba kwa mazingira ya Tanzania utaondoa usimamizi wa ujazi (Quantity) na badala yake utaangalia bei
“Lengo la Benki Kuu ni kudhibiti mfumuko wa bei ili kukuza uchumi wa nchi, riba itakuwa ni kiashiria cha mwenendo wa uchumi wa nchi.
” Mfumo huo mpya utazisaidia Benki kuimarika zaidi na kupanga riba.”amefafanua Dk.Missango
Kwa upande wa malengo ya Sera ya Fedha, Dk Missango alitanabaisha kuwa ni kuhakikisha kiwango cha fedha kilichopo kwenye uchumi kinakidhi mahitaji ya Shughuli zinazoendana na uchumi
“Kiwango kikubwa cha fedha katika mzunguko zaidi ya mahitaji ya shughuli za uchumi huongeza bei za huduma na bidhaa (inflation) wakati kiwango kidogo kisichokidhi mahitaji ya shughuli za kiuchumi husababisha kuzorotesha shughuli za uchumi, na kudumaza ukuaji wa wa uchumi, na hivyo, utekelezaji wa sera ya fedha unalenga kuweka utulivu wa bei za bidhaa na huduma na kuwezesha shughuli za uchumi kufanyika ipasavyo .” alihitimisha Dk Missango.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Sarafu, BoT, Ilulu Said amewataka wananchi kupeleka sarafu kwenye benki za biashara zilizo karibu nao ili wabadiishiwe na kupata noti.
Amesema, kwa sasa kampeni ya ukusanyaji sarafu inahusisha sarafu za Sh.50, 100 na 200.
“Sarafu za Tanzania zina uimara wa kutumika kwa a miaka 30 bila ya kuharibika kulingana na utunzaji wake, hivyo tunawahimiza wananchi wasikae na sarafu kwenye vibubu, wazipeleke kwenye benki wakazibadilishe ili wapewe noti
“Lengo ni kuwafikia watumiaji wengine kwenye mzunguko wa fedha.” ameongeza Ilulu.
Amesema mwishoni mwa mwaka jana BoT iliyaelekeza benki zote ya biashara kupokea sarafu kutoka kwa wananchi, lakini pia hata kwa wale ambao hawana akaunti kwenye benki hizo nao wapo huru kupeleka sarafu
“Katika kampeni hii tumeondoa vikwazo vya upokeaji wa sarafu hizo, awali tulielekeza sarafu chafu ndio zipelekwe kwenye mabenki, lakini kwa sasa benki zimeelekezwa kupokea sarafu zote, chafu na safi.” amesema.