NA TERESIA MHAGAMA,ZANZIBAR
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko,
amefungua Jengo la Afisi ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) lililoko
eneo la Madema, Zanzibar na kupongeza mafanikio na ushindi wa
kufanikisha miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar.
Dk Biteko amesema, kuelekea Kilele cha Mapinduzi ya Zanzibar, watu
waliopewa dhamana ya kusimamia miradi hiyo ambayo Serikali imepeleka
fedha nyingi, wafanye kazi kwa uaminifu kwani watatatoa hesabu si tu
kwa waliowaweka madarakani, au Wananchi bali kwa Mwenyezi Mungu,
hivyo wafanye kazi kwa uaminifu mkubwa.
“Nitoe wito kwenu ZAWA hakikisheni mnawahudumia vema Wazanzibari, ili
waone fahari ya kuhudumiwa na ninyi, na nitoe wito kwetu Sisi tuliopo
madarakani kuhakikisha tunatoa huduma kwa weledi wa hali ya juu kwa
maslahi ya Wananchi wetu” alisisitiza Dk Biteko
Aidha, alipongeza pia Wizara ya Maji kwa kuwajali wafanyakazi wake kwa
kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa wafanyakazi wake ikiwa ni
kuwajengea jengo lililoondoa changamoto ya nafasi kwa wafanyakazi
hususani kwenye jengo la awali.
Dk Biteko amesema, ujenzi wa Jengo Hilo la ghorofa none lililogharimu
kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 92.18 kama mkopo toka Benki ya
Exim Kutoka India kwa ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
unahusisha Ofisi za wafanyakazi, Maabara, Ukumbi wa Mikutano, Maegesho
na Ukumbi wa Mazoezi na kuipongeza Wizara ya Maji, Nishati na Madini
kwa kujenga jengo lenye hadhi na ubora wa hali ya juu.
“Niwashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassani na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt.
Hussein Ali Mwinyi kwa maono na miongozo yao iliyopelekea kukamilika
kwa miradi mikubwa na ya kimkakati yaani wanaupiga mwingi” amesisitiza
Dk. Biteko.
Awali, akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Waziri Maji,
Nishati na Madini Zanzibar, Shaibu Kaduara, amesema ujenzi wa
jengo hilo ni muendelezo wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo
Maji na tayari miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa ili kutatua
kero ya Maji visiwani Zanzibar na kuongeza kuwa wataendelea na kasi
hiyo bila kulala ili kuwaletea maendeleo wanachi wa Zanzibar.
Alimpongeza Dk. Biteko kwa ushirikiano ambao Zanzibar inapata
hususani kwa miradi ya Umeme hususani uimarishaji wa miundo mbinu ya
umeme, kwa kutekeleza mradi wa kuleta umeme kutoka Tanzania Bara,
kilovolt 220 kutoka Rasi Kilomoni na ule wa Pemba kwa Msongo wa
Kilovoti 132 na kuishukuru Serikali kwa Kufanikisha miradi hii.
“Zanzibar ndio nchi pekee Afrika Mashariki, na pengine Duniani kwa
kuwajali wananchi wake kwa kuwapatia Maji ambayo wanayachagia na sio
kulipia Maji” alisisitiza Kaduara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA)
Mhandisi. Dk. Salha Mohamed, amesema ujenzi wa jengo hilo ulianza
mwezi Machi, 2021 ikiwa ni sehemu ya uhuishaji na ustawishaji Maji
Zanzibar chini ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maji chini ya
miradi mitatu ambapo wa kwanza ni wa Mfenesini na Dole unaogharimu
Dola za Kimarekani Milioni 26,167, 200, Awamu ya pili unaogharimu
kiasi cha Dola za kimarekani Milioni 27,740,731, ambao umejenga
matanki makubwa sita, matatu chini, na matatu juu, na ya tatu ni ile
inayohusiaha Masongini, Kwarara na ZAWA kwa ujenzi wa matanki matano,
na unagharimu kiasi cha zaidi ya milioni 35.