NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL) limekanusha taarifa zilizoandikwa mitandaoni kwamba iliuziwa ndege Q300 Bombardier ikiwa tayari ni mbovu na imekwama huko Malta.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika hilo leo Januari 7,2024 ,ndege hiyo sio miongoni mwa ndege mpya zilizonunuliwa na Serikali ya Tanzania katika kipindi cha Mpango wa Ufufuaji wa ATCL ulioanza mwaka 2016.
“Ndege hii haikununuliwa na Serikali bali ni miongoni mwa ndege mbili zilizopatikana kupitia mbia aliyefanya uwekezaji kwa kuleta ndege mbili za aina ya Dash 8 – Q300 mwaka 2008 na kupewa usajili wa namba 5H-MWG na 5H-MWF kwa kufuatana.
“Ndege hizo za Q300 ziliundwa mwezi Mei 1997 na kabla ya kuwasili nchini zilikuwa zimetumika kwa takribani miaka 11, hata hivyo Kampuni ya Bombadier (Manufacturer) ilisitisha uundwaji wake tangu Mei 2009.
“Ndege zilizonunuliwa na Serikali kuanzia mwaka 2016 ni ndege 13 ambazo ni Q400 – Bombadier (5), Airbus A220-300 (4), Boeing 787-8 (2), Boeing 767-300F (1) na Boeing 737 MAX – 9 (1), ATCL ilibakiwa na ndege ya Q300 moja yenye usajili wa namba 5H-MWF.
“Baada ya ndege yenye usajili wa namba 5H-MWG kupata ajali mwaka 2012 na kushindikana kutengenezeka kutokana na ukubwa wa uharibifu wa ndege hiyo.
“Ndege iliyobakia iliendelea na safari zake hadi mnamo Mei 2017 baada ya waundaji (Manufacturer) wa ndege hizi kuagiza kuwa ndege zote za aina hii duniani zisiendelee na safari hadi zitakapofanyiwa matengenezo ya lazima ya matenki ya mafuta kwa ajili ya usalama, sanjari na agizo hilo.
“Ndege hii pia ilihitaji kufanyiwa matengenezo makubwa yanayojulikana kitaalamu kama 6C-Check ambapo ilifika nchini Malta mwezi Novemba 2020 kwa ajili ya matengenezo hayo.
“Kutokana na changamoto ya upatikanaji wa vipuri iliyosababishwa na athari za UVIKO 19 ambapo wazalishaji wa vipuri walipunguza na wengine kuacha utengenezaji wa vipuri kumesababisha matengenezo hayo kutokamilika kwa muda uliotarajiwa.
“Ndege hii inatarajiwa kurejea nchini baada ya kukamilika kwa matengenezo hayo, ATCL inawaomba wadau wake kupuuza taarifa za uzushi zinazosambazwa mitandaoni zenye lengo la upotoshaji,”imefafanua taarifa iliyotolewa na ATCL.