- PESA sawa na ulimi, inageuzwa geuzwa,
Yazidi nyama ulimi, vile inavyotukuzwa,
Ni zaidi ya usomi, pesa vile ukijazwa,
Pesa ndumilakuwili, ni njema tena ni mbaya. - Yawatafuna wasomi, vile inavyotukuzwa,
Wanashikwa na vichomi, endapo hawajajazwa,
Ikiwepo hawagomi, vile wanavyotulizwa,
Pesa ndumilakuwili, ni njema tena ni mbaya. - Ukisikika uvumi, au kwa kunong’onezwa,
Madini yenye uchumi, huko yameshachokozwa,
Wasosoma na wasomi, hawawezi kutulizwa,
Pesa ndumilakuwili, ni njema tena ni mbaya. - Mwenye pesa hasimami, njiani akaulizwa,
Pesa zampa utemi, hata anapochokozwa,
Masikini kama mimi, ndiye unapatilizwaa,
Pesa ndumilakuwili, ni njema tena ni mbaya. - Mwenye pesa ni msomi, bila hata kuelezwa,
Mambo yote ya kisomi, kupata hajakatazwa,
Anaajiri na wasomi, auliza aelezwa,
Pesa ndumilakuwili, ni njema tena ni mbaya. - Wahujumu wa uchumi, pesa wataka kujazwa,
Tena wengine wasomi, wafanya yalokatazwa,
Wanautaka utemi, haki yote yapuuzwa,
Pesa ndumilakuwili, ni njema tena ni mbaya. - Wahongaji hawavumi, yao yaweze penyezwa,
Rushwa hiyo hawakomi, ambayo imekatazwa,
Wakishikwa zao ngumi, gerezani wanalazwa,
Pesa ndumilakuwili, ni njema tena ni mbaya. - Pesa sadaka ya mimi, kanisani yatukuzwa,
Inaongeza uchumi, taifa laendelezwa,
Pesa inao uvumi, haiwezi telekezwa,
Pesa ndumilakuwili, ni njema tena ni mbaya. - Kutafuta hatukomi, ndivyo tunavyohimizwa,
Pesa nguvu ya ulimi, ikiwepo twatukuzwa,
Tukitafuta kitemi, mwishoni tutaunguzwa,
Pesa ndumilakuwili, ni njema tena ni mbaya. - Tuachane na uvumi, kufanya yalokatazwa,
Kwa elimu na usomi, tufanye yakutukuzwa,
Pesa nyama ya ulimi, haifai telekezwa,
Pesa ndumilakuwili, ni njema tena ni mbaya.
Na Lwaga Mwambande
lwagha@gmail.com 0767223602