NA TERESIA MHAGAMA, BUKOMBE
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko
amewapongeza na kuwashukuru Walimu wote wanaofundisha shule za Msingi
na Sekondari wilayani Bukombe kwa kuwajali wanafunzi na kuwafundisha
kwa weledi na maarifa ambayo yamepelekea wilaya hiyo kuwa na ufaulu
mzuri.
Dk.Biteko ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, amesema hayo wakati
akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kabuhima, Kata ya Uyovu wilayani
Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya ziara zake kwenye maeneo
mbalimbali katika Jimbo la Bukombe.
“ Nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru Walimu wote
katika wilaya ya Bukombe, wametupa heshima kubwa, miaka ya nyuma
ambayo ni 2015 kurudi nyuma, hata tulipokuwa tukipangwa kimkoa katika
matokeo ya Darasa la Saba, Kidato cha Nne na Kidato cha Sita tulikuwa
katika nafasi ya mwisho, leo Walimu wa wilaya yetu wamefanya kazi
kubwa, wametuheshimisha kwani katika Mkoa kama hatuwi wa kwanza, basi
tunakuwa wa Pili.” amesema Dk.Biteko
Amesema kuwa, ufaulu huo mzuri unatokana na walimu hao kuwajali
Wanafunzi, kuwafundisha vizuri na hivyo kupelekea wanafunzi hao
kufanya vizuri katika mitihani yao, hivyo amesisitiza suala la wazazi
na walezi kuwapeleka watoto wao shule na wasiwavunje moyo pale
wanapoona hawafanyi vyema katika masomo.
Aidha, Dk Biteko amekea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi
kutopeleka watoto shule kwa nia ya kuwaozesha na kupata mahari,
amesema kuwa Dkt. Samia Samia Suluhu Hassan amejenga na anaendelea
kujenga shule za ngazi mbalimbali nchini hivyo wajibu wa wazazi ni
kupeleka watoto shule na siyo kuwakwamisha.
Katika Kata hiyo ya Uyovu, Dk.Biteko amesema kuwa, miradi mbalimbali
ya maendeleo inaendelea kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa Shule za msingi
na Sekondari, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami na ujenzi wa taa
za barabarani utakaoanza mwezi Januari mwaka 2024 ikiwa ni utekelezaji
wa ahadi ya Rais, Dkt. Samia aliyoitoa kwa wakazi wa Kata hiyo.
Katika hatua nyingine, Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dk.Biteko amezindua wodi mpya katika Hospitali ya
Kumbukumbu ya Charles Kulwa iliyoko Runzewe wilayani Bukombe ambapo
wodi hiyo ni maalum kwa ajili ya kuhudumia wanawake wajawazito
wanaofanyiwa upasuaji.
Akiwa hospitalini hapo, DkBiteko alipata fursa ya kutembelea
maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo iliyoanzishwa mwaka 1992 ikiwa
kama Zahanati, mwaka 2005 ilipanda hadhi ya kuwa Kituo cha Afya na
mwaka 2020 ilipandishwa hadhi ya kuwa hospitali ya Wilaya, ambapo
aliupongeza uongozi wa hospitali hiyo inayohudumia wagonjwa takribani
elfu 72 kwa mwaka.
Awali, akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Martine Shigella ambaye alikuwa mgeni maalum, alimshukuru Rais, Dk
Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kuinua sekta Afya
katika Mkoa wa Geita na maeneo mengine nchini akitolea mfano ujenzi wa
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato.
Aliwataka wadau wengine kuiga mfano wa wamiliki wa hospitali hiyo kwa
kuhudumia wagonjwa wengi na kutoa huduma kwa kiwango cha hali ya juu
hadi kufikia hatua ya kupandishwa hadhi.