NA TERESIA MHAGAMA, ROMBO
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko leo Desemba 23, 2023
ameshiriki mashindano ya Rombo Marathon yaliyohusisha mbio za Kilometa
5, 10 na 21 na kupongeza waandaaji kwa ubunifu wao uliosababisha
Mbio hizo kuendelea kuimarika kila mwaka ambapo licha ya kulenga
katika kuimarisha afya kwa washiriki, imejikita katika kuchangia
uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii na utunzaji wa mazingira.
Dk Biteko ametoa pongezi hizo wilayani
Rombo mkoani Kilimanjaro, akiwa ni mgeni rasmi katika mbio hizo
ambapo alikimbia kwa umbali wa kilometa tano akiambatana viongozi
mbalimbali wa Kitaifa, Mkoa na Wilaya.
“Nimeelezwa kwamba lengo la Rombo Marathon ni kuhamasisha utunzaji wa
mazingira, kukuza utalii wa ndani, kuchangia fedha kwa ajili ya shule
za msingi na Sekondari wilayani Rombo ili ziweze kuwa na vyoo salama
na pia kuchangia fedha zitakazowezesha kupandisha hadhi ya hospitali
ya Huruma wilayani Rombo ili iweze kuwa hospitali ya Rufaa,
niwapongeze sana kwa jambo hili lenye manufaa.” amesema Dk.Biteko
Ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali
zinazofanywa na wananchi katika kujiletea maendeleo ikiwemo kuunga
mkono uanzishaji wa maeneo ya huduma za kijamii kama vile Shule, Vituo
vya afya n.k
Ameongeza kuwa, Rombo Marathon licha ya kuchangia katika kuboresha
huduma za kijamii, washiriki wa ndani na nje ya nchi pia wamepata
fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika nyanja mbalimbali
ikiwemo za kiuchumi na kijamii.
Dk. Biteko, amempongeza Mbunge wa Rombo ambaye pia ni Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kwa kuanzisha
mbio hizo ambazo sasa zinafanyika kwa mara ya Pili huku akieleza
kuwa ubunifu huo unapaswa kuigwa na kufanyika katika maeneo mbalimbali
nchini.
Katika hatua nyingine, Dk Biteko amepongeza utamaduni wa watanzania
wanaotoka mkoani Kilimanjaro wa kurudi katika maeneo yao wakati wa
sikukuu za mwisho wa mwaka huku akieleza kuwa kurudi nyumbani
kunasaidia kufahamu changamoto zilizopo na kuzitatua akitoa wito kwa
wananchi wa maeneo mbalimbali kuwa na utamaduni huo.
Mbunge wa Rombo ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Profesa Mkenda amesema kuwa, mbio hizo hufanyika kila mwaka
Desemba huku ikiwa na malengo maalumu ambayo ni chanya
kwa jamii.
Amemshukuru, Dk Doto Biteko kwa kuheshimu mbio hizo na kukubali
kushiriki akieleza kuwa ushiriki huo utakuza marathon hiyo na
kuiimarisha si kiwilaya tu, bali kimkoa na kitaifa.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria marathon hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Nurdin Babu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi
Felchesmi Mramba na .Dk Tausi Kida, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Mipango na Uwekezaji.
Washindi wa Kilometa 21 katika mbio za Wanawake ni Neema Mswadi (3),
Nathalie Elisante (2) na Sara Ramadhan (1).Washindi wa Kilometa 21
Wanaume ni Agustino Sule (3), Nestory Steven (2) na Chigale Giniki
(1).