NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)
1.TUMEOANA ni kweli, Mwenza ninajivunia,
Tuwamoja si wawili, Kiapo chatuambia,
Nyumbani mbona hulali, Baridi waniachia?
Hayo wala si mapenzi, Mwenzangu nakuambia.
2.Kumbuka tulikotoka, Vile nilijisikia,
Wawili tulipotoka, Yetu kwenda jifanyia,
Mbona umebadilika, Mawazo waniachia?
Hayo wala si mapenzi, Mwenzangu nakuambia.
3.Pesa wewe wazipata, Na mimi najipatia,
Zamani tukizipata, Kazi tulizifanyia,
Mbona sasa ukipata, Mbali ndiko zaishia?
Hayo wala si mapenzi, Mwenzangu nakuambia.
4.Tumejaliwa watoto, Shule wanahudhuria,
Kila siku kuna wito, Ada hujawalipia,
Mbona wanipa majuto, Uzee sijafikia?
Hayo wala si mapenzi, Mwenzangu nakuambia.
5.Pesa zako ni za kwako, Yako unajifanyia,
Hivi ni wa ndoa wako, Au ni mpita njia?
Liko wapi penzi lako, Goti ulinipigia?
Hayo wala si mapenzi, Mwenzangu nakuambia.
6.Sikukuu imefika, Wapi kwakukimbilia?
Je watoto watacheka, Au watajililia?
Hivi kitaeleweka, Sisi tubaki twalia?
Hayo wala si mapenzi, Mwenzangu nakuambia.
7.Napita barabarani, Miye bado navutia,
Na ningekutia soni, Kwa buzi kujipatia,
Kwa Mungu siyo thamani, Kisasi kulipizia,
Hayo wala si mapenzi, Mwenzangu nakuambia.
8.Ni kipindi cha mpito, Japo sana naumia,
Ningekuwa na kipato, Na usingenisikia,
Ningesomesha watoto, Na yangu kujifanyia,
Hayo wala si mapenzi, Mwenzangu nakuambia.
9.Vile ninabangaiza, Wewe unanichunia,
Una pesa umejaza, Ukwasi wajivunia,
Mbona unajisogeza, pesa zikikuishia?
Hayo wala si mapenzi, mwenzangu nakuambia.
10.Sasa nakata rufaa, Mungu wangu namwambia,
Nasema umekataa, Kiapo kushikilia,
Tena kwako sitakaa, Nisije moyo umia,
Hayo wala si mapenzi, Mwenzangu nakuambia.
lwagha@gmail.com 0767223602