NA MWANDISHI MAALUMU, DAR ES SALAAM
BALOZI wa Tanzania nchini Cuba Humphrey Polepole amesema kuwa atashirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuhakikisha watanzania wanaendelea kupata huduma bora za matibabu ya moyo.
Balozi Polepole ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipotembelea Taasisi hiyo kwaajili ya kuona namna ambavyo nchi ya Cuba inaweza kushirikiana na Tanzania katika utoaji wa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo.
Alisema nchi ya Cuba imepiga hatua kubwa katika sekya ya afya na kuna madaktari wengi wa Tanzania wamesoma nchini humo, ataangalia namna ambavyo madaktari bingwa wa moyo kutoka nchini Cuba watashirikiana na madaktari bingwa wa JKCI katika kutoa huduma ya tiba bobezi kwa wananchi.
“Nchi ya Cuba ina viwanda vingi vinavyotengeneza vifaa tiba mbalimbali vikiwemo vya moyo kwa bei naafuu ukilinganisha na soko la dunia, nitaangalia namna ya kuwaunganisha na viwanda hivi ili muweze kununua vifaa hivyo ambavyo vitawasaidia wananchi”, alisema Balozi Polepole.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk. Peter Kisenge alimshukuru Balozi Polepole kwa kuitembelea Taasisi hiyo na kusema kuwa wataendelea kushirikiana naye katika kuboresha huduma za afya ya moyo kwa watanzania.
“Taasisi yetu imekuwa na ushirikiano mzuri na Balozi Polepole kwani wakati yuko nchini Malawi alifanikisha kujenga mahusiano yaliyowezesha wataalamu wetu kwenda nchini humo kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi. Hivi sasa tunapokea wagonjwa wengi kutoka nchini Malawi ambao wanakuja kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo”.
“Ninaamini kuwepo kwake nchini Cuba Taasisi yetu itafaidika kwa wataalamu wetu kujengewa uwezo zaidi na kupata vifaa tiba vya matibabu ya moyo”, alisema Dk.Kisenge.