NA MWANDISHI MAALUMU, RUANGWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ruangwa leo Alhamisi, Desemba 21, 2023 amefanya ziara kwenye vijiji vinne vya kata ya Chingumbwa, Mkutingome, Naunambe na Mbekenyera wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Akiwa katika ziara hiyo Majaliwa ameagiza Mamlaka ya Maji Safi na Salama (RUWASA )Wilaya ya Ruangwa kukamilisha kwa wakati mradi wa maji utakaohusisha vijiji vya Chingumbwa na Mkutingome ili wananchi hao waanze kupata huduma ya maji safi na salama.
Akitoa maelezo kuhusu mradi huo, Kaimu Meneja wa RUWASA, wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Rashid Shabani amesema kuwa wanaendelea na taratibu za ujenzi wa mradi huo ambao unategemea kuzalisha zaidi ya lita 5,000 kwa saa.
Pia amewataka wakazi wa vijiji hivyo kuendelea kuwa na imani na Serikali ya awamu ya sita kwani imedhamiria kutatua kero zao.
“Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati ya kushirikiana na wana-Ruangwa na Watanzania wote katika kutatua changamoto zilizopo hivyo endeleeni kuwa na imani naye, na muwe na imani na Serikali yenu ya awamu ya sita,” amesema.
Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chingumbwa katika kata ya Mbekenyera, Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka miwili, kata hiyo imepatiwa Sh. Bilioni 2.5 za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya sekta za afya na elimu.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu ujenzi na ubora kwenye sekta ya elimu kuanzia shule ya msingi ili watoto wasitembee umbali mrefu kufuata shule.
Ili kuharakisha kukalimika kwa mradi huo, Waziri Mkuu amesema: “Natambua kuwa ujenzi huo utahusisha uwekaji wa vilula, kazi hii msiitoe kwa mkandarasi mmoja, gaweni kazi, mmoja apewe chanzo tu, mwingine njia za maji na mwingine ajenge vilula,”
“Hadi sasa tumeshafanya tafiti na kuchimba kisima na tunaendelea na kuangalia ubora wa maji, yote haya tutayafanya katika mwaka huu wa fedha,” amesema.
Akiwa kijiji cha Naunambe, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Nambawala na kusema ameridhishwa na ubora wa viwango vya ujenzi wa shule hiyo.
Amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma aendelee kuwatumia Wakandarasi hao.
Katibu wa mradi huo, Hussein Omari alisema Juni 30, mwaka huu, Kata ya Mbekenyera, ilipokea Sh.Milioni 560.5 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya chini ya Programu ya Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambapo hadi sasa zimetumika sh. milioni 510. Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Desemba 30, 2023.
Akiwa kijiji cha Mbekenyera, Waziri Mkuu alitembelea kituo cha afya na kukagua utoaji wa huduma kwenye kituo hicho. Alimwagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Boniface Nonga afuatilie matengenezo ya gari la wagonjwa ili liweze kuwahudumia wananchi wa vitongoji vya jirani.
Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho, aliwasisitiza vijana wa kata hiyo watumie fursa ya uwepo wa madini ili kukuza uchumi wao na waende Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ili wapate ujuzi na kuboresha stadi kwenye uchimbaji wa madini.
“Vijana, akinamama, na wazee wenzangu, tuna fursa ya madini ya graphite (bunyu), tujipange kuanza kunufaika na fursa hii, vijana nendeni mkaongeze ujuzi VETA, fungueni maduka, jengeni nyumba za wageni, kwani madini ni uchumi.”