NA MWANDISHI WETU, SIHA
MKUU wa Wilaya ya Siha Dk. Christopher Timbuka amewahimiza wakazi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Huduma hizo za kibingwa zinatolewa katika kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo ya siku tano inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya wilaya ya Siha.
Dk Timbuka alitoa rai hiyo jana wakati akizungumza na timu ya wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) waliofika ofisini kwake kwaajili ya kujitambulisha.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya aliishukuru JKCI kwa kuwatuma madaktari bingwa pamoja na wataalamu wa lishe ambao wanatoa huduma kwa wananchi pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali ya wilaya ya Siha.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda aliushukuru uongozi wa wilaya ya Siha kwa kuwakea na kukubali kushirikiana na hospitali ya wilaya hiyo katika kutoa huduma za matibabu kwa wananchi.
Nkinda alisema Taasisi hiyo imekuwa ikitoa huduma ya tiba mkoba ya kuwafuata wananchi mahali walipo ijulikanayo kwa jina la Dk Samia Suluhu Hassan Outreach Services kuwepo kwa huduma hiyo kumesaidia wananchi wengi hasa wa mikoa ya pembezoni kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.
Nao wananchi waliopata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa licha ya kuwapunguzia gharama ya safari ya kuifuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam pia wamefahamu afya ya mioyo yao ikoje.
Huduma hizo za uchunguzi na matibabu ya moyo zinatolewa bila malipo yoyote yale ambapo wananchi wanapimwa kiwango cha sukari kwenye damu, shinikizo la damu, uwiano baina ya urefu na uzito , kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO) na mfumo wa umeme wa moyo (ECG).