NA TERESIA MHAGAMA, MWANZA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema ameridhishwa na maendeleo mazuri ya mradi wa maporomoko ya umeme wa Rusumo wa Megawati 80 ambapo
utazalisha Megawati 80 na kila nchi
itapata Megawati 27 za umeme.
Mradi huo unatekelezwa kwa pamoja na nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi
umefikia asilimia 99.9 na nchi hizo tayari zimeanza kupata umeme.
Aidha Biteko alitumia fursa kuipongeza Bodi na Watendaji kutoka kampuni ya umeme ya Rusumo na
wakandarasi kwa usimamizi na utekelezaji wa mradi huo.
Haya yamejiri jijini Mwanza wakati Dk Biteko akiongoza kikao cha ngazi ya Mawaziri wa Nishati ambaye yeye ni
Mwenyekiti wa Mawaziri wa wanaosimamia mradi huo kutoka nchi hizo Tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi.
Wakati hio huo, Biteko alisema Mawaziri hao wamekubaliana kuwa, mradi huo uzinduliwe mwezi Machi mwaka 2024 hivyo wamemtaka Mkandarasi kukamilisha mradi huo mapema na atoe cheti cha kukamilisha mradi.
Alisema uzinduzi huo utafanyika katika eneo la mradi huku mwenyeji wa
shughuli hiyo akiwa ni Tanzania.
Alisema kuwa, mradi huo una umuhimu kwa nchi zote tatu kwani bado
nchi hizo zina changamoto ya upatikanaji wa uhakika wa umeme hivyo
kukamilika kwa mradi huo kutapunguza changamoto hizo na kuongeza
uimara kwenye gridi.