NA MWANDISHI WETU, NGORONGORO
MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inakanusha taarifa zilizosambaa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii kuhusu vifo vya mifugo ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na kula chumvi yenye sumu.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Oktoba 7, 2023 na Kassim Nyaki Ofisa Uhifadhi Mwandamizi
Kitengo cha Uhusiano wa Umma – NCAA, habari zilizotolewa na baadhi ya mitandao hiyo kuhusu mifugo kupewa chumvi yenye sumu iliyonunuliwa na Mamlaka si za Kweli.
Taarifa ya Nyaki ilieleza kuwa, Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuanzia mwaka 2017 imekuwa ikitoa chumvi katika vijiji vitano (Misigyo, Kayapus, Mokilal, Oloirobi na Irkepus) vinavyopakana na Bonde la Ngorongoro kama mbadala wa kuzuia mifugo iliyokuwa inaingia ndani ya bonde la Kreta kwa ajili ya kulamba madini chumvi.
Tangu Serikali ianze kutoa madini chumvi kwa wananchi kwa ajili ya mifugo yao, hakujawahi kuwa na uthibitisho wa Kitaalam na Kisayansi kuhusu kuathirika kwa mfugo wowote baada kutumia chumvi iliyogawiwa.
Picha zinazosambazwa kwenye baadhi ya mitandao zikionesha Mizoga ya mifugo iliyokufa ni za mwaka 2022 ambapo baadhi ya mifugo iliathirika na kufa kutokana na athari za ukame.
Kutokana na Sensa iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2017, idadi ya Mifugo ndani ya eneo la Hifadhi ilikuwa ni 809,459 (Ng’ombe 238,826, Mbuzi 226,260 na Kondoo 344,373).
Ongezeko hili la mifugo sambamba na upungufu wa malisho kunapelekea mifugo iliyopo kutokuwa na afya bora ambayo inaweza kuhimili kipindi cha ukame.
NCAA inaomba wananchi kupuuza taarifa hizi kwa kuwa si za kweli na Serikali kupitia NCAA inaendelea kutekeleza majukumu yake ya Uhifadhi, Utalii na maendeleo ya Jami kwa kufuata sheria, kanuni, na misingi ya haki za binaadamu.