NA DANSON KAIJAGE,MEATU
MKURUGENZI wa Miradi kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) Mhandisi , Boniface Mkumbo amesema mradi wa ujenzi wa barabara ya kilometa 25 kwa kiwango cha lami na mwingiliano wa Daraja la sibiti ambao utatekelezwa na Mkandarasi CHICO na kusimamiwa na TECU kwa gharama ya Sh. Bilioni 21.776 upo mbioni kuanza.
Mhandisi huyo ametoa taarifa hiyo kwa Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa alipokuwa akifanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Ameongeza kuwa muda wa utekelezaji wa mradi ni miezi 18 ikijumuisha miezi 3 ya maandalizi na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari, 2025.
Mhandisi Mkumbo amesema kuwa sehemu ya barabara hiyo ni mchepuo wa barabara kuu kusini ma Serengeti inayoanzia Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti – Ng’amhuzi (Meatu) – Lalago – Maswa ambayo yenye urefu wa kilometa 389.
Kwa msisitizo zaidi Waziri wa Ujenzi, Bashungwa amesema kuwa ujenzi wa barabara ya maingilio katika Daraja la Sibiti zenye urefu wa kilometa 25 kwa kiwango cha lami tayari umeanza na upo katika hatua za awali za utekelezaji.
Amesema Ujenzi wa barabara hiyo wenye kilometa 5 upande wa Wilaya ya Meatu na Kilometa 20 upande wa Wilaya ya Mkalama ni kiungo muhimu kwani zitaunganisha mikoa ya Singida na Simiyu.
Bashungwa ameeleza hayo Oktoba 6, 2023 mkoani Singida wakati alipofika kukagua daraja la Sibiti (mita 82) ambalo ujenzi wake umekamilika na kumtambulisha mkandarasi wa Kampuni ya CHICO ambaye atatekeleza barabara za maingilio.
Amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa mikoa ya Arusha, Manyara, Singida na Simiyu.
Sambamba na hilo, Bashungwa ameeleza Dira ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mtandao wa barabara ambapo jumla ya kilometa 2,035 za barabara kwa kiwango cha lami zinatarajiwa kujengwa na tayari mikataba ya ujenzi wa barabara hizo zimeshasainiwa kwa utaratibu wa EPC + F.
“Moja ya mkakati wa Mhe. Rais katika kuongeza ufanisi katika Sekta ya usafirishaji ni pamoja na kuamua kuijenga barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti – Ng’amhuzi (Meatu) – Lalago – Maswa (km 389)” amesema Bashungwa
Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ipo katika hatua za kumpata mkandarasi wa kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Iguguno – Nduguti – Sibiti – Gumanga – Chemchem (km 89) mara baada ya usanifu wake kukamilika mkoani Singida