NA WMJJWM, DODOMA
SERIKALI imesema inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ‘NGOs’ ili kutekeleza majukumu yake na mchango wake kwa jamii.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dk. Dorothy Gwajima wakati akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dodoma Septemba 27, 2023 kuelekea Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali litakalofanyika Oktoba 03 hadi 05, 2023 jijini Dodoma
Dk. Gwajima amesema jitihada za Serikali ni kutengeneza Ramani ya Kidigitali ya Utambuzi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kukabiliana na changamoto ya kiutendaji ya Mashirika hayo na utekelezaji wa miradi na afua zinazofanana ndani ya eneo moja.
“Wizara kwa kushirikiana na wadau iliamua kuboresha Mfumo wa Kielektroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuongeza Ramani ya Utambuzi wa Mashirika kwa njia ya kidijitali ambapo ramani itasaidia Wadau, Taasisi za Kiserikali, Sekta Binafsi na Jamii kupata taarifa za Mashirika kwa urahisi.” amesema Gwajima.
Akitaja faida za kuwepo kwa Ramani ya Utambuzi wa Mashirika kwa njia ya kidijitali amesema ni pamoja na kujua mahali au eneo shirika lilipo; kujua eneo la utekelezaji wa miradi ya Mashirika (thematic area), afua zinazotekelezwa, wanufaika wa mradi, mchango wa mashirikia upande wa ajira zilizotolewa na Mashirika hayo.
Faida zingine ni kuuliza na kupata majibu ya moja kwa moja kujua fursa zilizopo, kujua Mashirika yaliyokiuka vigezo vya usajili wake, kutambua mchango wa Mashirika kupitia fedha za miradi, kujua idadi ya Mashirika kwenye kila Mkoa, Wilaya na Halmashauri na kujua miradi inayotekelezwa kwa wingi au uchache katika Mikoa.
“Ramani hii itawezesha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji ili kuleta maendeleo endelevu nchini na mchango wake kuonekana bayana kwa Maendeleo ya Taifa,” ameongeza Dk. Gwajima.
Wakati huo huo Waziri Dkt. Gwajima amesema, Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) imeandaa Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali litakalofanyika kuanzia tarehe 03 – 05 Oktoba, katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Lengo kuu la Jukwaa ni kuimarisha Mahusiano baina ya Serikali, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wadau wengine pamoja na kutambua mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa maendeleo ya Taifa,” amesema
Kwa mwaka huu wa 2023, Jukwaa hilo litajumuisha washiriki zaidi ya 2000 huku Kaulimbiu ikiwa ni Mashirika Yetu, Maadili Yetu, Taifa Letu.