NA WAANDISHI WETU, GEITA
*AIAGIZA REA KUELEKEA VIJIJINI
*AIPONGEZA REA KWA KUELEWA DHAMIRA YA RAIS KUPELEKA UMEME VIJIJINI
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko ameanza kazi ya kuwasha umeme vijijini ambapo leo amewasha umeme katika Kijiji cha Ihako, wilayani Bukombe mkoani Geita na hivyo kuwezesha wananchi katika kijiji hicho kuanza kutumia rasmi nishati hiyo.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho, Dkt. Biteko amepongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi nzuri ya kupeleka umeme vijijini ikiwemo kijiji cha Ihako na kuelekeza kuwa, sasa mwendo ni wa mchakamchaka kupeleka umeme kwa wananchi wote waliopo vijijini.
“REA nendeni vijijini, muda wa kufanya vikao kwenye maukumbi makubwa, au makao makuu ya miji hatutaki, tunataka tuwaone mnaenda vijijini kupeleka umeme, nyie ni Wakala wa Nishati Vijijini siyo Wakala wa umeme mijini , vikao vyenu viwe na wananchi na magari yenu yapite humo wanamopita wananchi wenye maisha ya kawaida kabisa, ” amesisitiza Dk. Biteko
Ameongeza kuwa, Serikali inataka kuona shuguli za kupeleka na kuwasha umeme vijijini zinatokea, na kwamba umeme huo uingie kwenye nyumba zote bila kubagua kwani kila mwananchi anahitaji umeme.
Aidha ameelekeza kuwa, mahali penye changamoto za umeme zitatuliwe kwa haraka na si kumsubiri, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutatua changamoto wakati wa ziara zake wakati wasaidizi wake wapo.
Amesema kuwa fedha za kupeleka umeme vijijini zipo ambazo zimechangiwa na wananchi, Serikali na wadau wa maendeleo hivyo hakuna sababu ya kukwamisha miradi ya umeme nchini.
Kuhusu nishati safi ya kupikia, amesema kuwa, Serikali inataka ione wananchi wanatumia nishati hiyo na kwamba REA waweke mpango ili mitungi ya gesi iwafikie wananchi wa kawaida nchini na hivyo kuwaondolea matumizi ya nishati ambayo si salama.
Vilevile amesema kuwa, Serikali inafanya jitihada mbalimbali ili kupata umeme wa kutosha kutoka vyanzo vya umeme ikiwemo Mradi wa Julius Nyerere ( MW 2115) ambao utaongeza kiasi kikubwa cha umeme kwenye gridi ya Taifa na hivyo wadau wa umeme watapata umeme wa kutosha ikiwemo viwanda, wachimbaji wadogo na wenye shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema kuwa, Mkoa wa Geita una jumla ya Vijiji 461 ambapo vijiji 399 sawa na asilimia 86.6 vimepata huduma ya umeme kupitia miradi ya REA Awamu ya Tatu mzunguko kwanza, REA Awamu ya Pili na REA Awamu ya Kwanza.
Amesema kuwa, REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali mkoani Geita ambapo wakandarasi wapo maeneo ya miradi wanaendelea na kazi na kuitaja miradi inayoendelea kuwa ni REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, mradi wa kupeleka umeme pembezoni mwa miji Awamu ya Tatu , mradi wa kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo pamoja na mradi wa kupeleka umeme kwenye vituo vya afya na pampu za maji.