NA MWANDISHI WETU
Klabu ya soka ya Yanga ya jijini Dar es Salaam imetakata mjini Kigali, Rwanda baada ya kutoka kifua mbele kwa magoli 2-0 dhidi ya wapinzani wao El Marreikh ya Sudan.
Yanga ikicheza kwa kujiamini kama ipo nyumbani ilikosa magoli mengi kipindi cha kwanza hali iliyofanya mpaka timu hizo zinakwenda mapumziko, ubao ulisoma 0-0.
‘Super Sub’ Kennedy Musonda raia wa Zambia aliwainua wananchi kwa kukwamisha wavuni mpira kwa kichwa akiwa katikati ya msitu wa mabeki wa wapinzani wao.
Kinda Clement Mzize alipiga msumari wa mwisho baada ya kuitumia vema pasi ya mwisho aliyotengewa na Ki Aziz kwenye 18 ya wababe hao wa Sudan.
SIMBA YAIKOMALIA POWER DYNAMOS
Wakati watani wao Yanga wakiwa kibaruani Rwanda, Wekundu wa Msimbazi walikuwa Zambia wakipapatuana na wababe wa nchi hiyo Power Dynamos.

Simba wakiwa makini kila dakika waliruhusu goli la kwanza kutoka kwa wapinzani wao. Mpaka timu hizo zinakwenda mapumziko, Mnyama alikuwa nyuma kwa goli moja.
Baleke aliisawazishia Simba lakini Power Dynamos wakaweka chuma ingine na kufanya Simba wawe nyuma kwa goli moja.
Triple C, mwamba wa Lusaka Clautus Chama aliisawazishia Simba dakika za lala salama na kuwaacha wapinzani wao wakiwa mdomo wazi.
Mpaka refa anapuliza kipenga cha mwisho, timu hizo zilitoshana nguvu kwa magoli 2-2.
Mechi zote mbili ni za kuwania kombe la Klabu Bingwa barani Afrika. Marudiano yatafanyika jinini Dar es Salaam.