NA MWANDISHI WETU, MARA
SERIKALI imepanga kuunganisha mfumo wa utoaji wa leseni wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Tamisemi), lengo likiwa ni kurahisisha upatikanaji wa leseni za biashara.
Kwa mujibu wa Sheria, Brela inatoa leseni za kundi A ambazo ni za biashara za kitaifa na kimataifa ikiwemo za viwanda wakati Tamisemi ikitoa leseni za kundi B ambazo ni za biashara zisizo na sura ya kitaifa na kimataifa.
Akizungumza mjini Musoma Juni 26, 2023 wakati wa mafunzo maalumu kwa Maofisa Biashara kutoka halmashauri mbalimbali nchini, Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Leseni za Biashara kutoka Brela, Tawi Kilumile amesema mchakato wa kuunganisha mfumo huo utakamilika karibuni.
Mafunzo hayo yanahudhuriwa na Maofisa Biashara kutoka halmashauri za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tabora, Kigoma, Geita, Shinyanga, Mwanza, Kagera na wenyeji Mara.
“Kufika mwaka ujao wa fedha, mfumo utakuwa tayari kuwezesha leseni kutolewa kwa njia ya mtandao kote kuanzia zile za Brela ambazo tulianza kutoa kwa njia ya mtandao tangu mwaka 2018 na zile za ngazi ya halmashauri,” amesema Kilumile
Amesema utoaji wa leseni za Brela kwa njia ya mtandao umeboresha utekelezaji kwa kuongeza idadi ya leseni mpya kutoka 9, 200 mwaka 2018 hadi kufikia leseni 14, 000 mwaka jana.
“Utoaji wa leseni kwa njia ya mtandao siyo tu unarahisisha upatikanaji wa takwimu ya halisi ya biashara nchini, bali pia hupunguza gharama za biashara na kuokoa muda,” amesema
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka amewaagiza Maofisa Biashara wa halmashauri kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi kuwezesha ufunguaji na uendeshaji wa biashara katika maeneo yao na hatimaye kuongeza makusanyo na mapato ya ndani.
“Sekta ya biashara ni injini ya ukuaji wa uchumi, jamii na Taifa; wenye dhamana ya kuisimamia watimize wajibu, wawe ubunifu huku wakizingatia weledi na uzalendo. Lazima wawe wawezeshaji badala biashara,’’ amesema Chikoka
Musa Misana, mmoja wa wafanyabiashara Manispaa ya Musoma amesema utaoji wa leseni zote kwa njia ya mtandao siyo tu utaondoa urasimu, bali pia utawezesha na kusaidia biashara nyingi kufunguliwa na hatima makusanyo na mapato zaidi yatakayosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na huduma kwa jamii.
“Leseni kwa njia ya mtandao utaondoa mazoea ya kukutana na uso kwa uso na hivyo kumaliza changamoto ya vitendo vya rushwa katia utoaji wa leseni,’’ amesema mfanyabiashara mwingine mjini Musoma, Shamsa Ramadhani