NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
JARED Ojweke ameibuka mshindi wa gari aina ya Toyota Crown katika awamu ya pili ya kampeni ya Simu ni Simbanking ya Benki ya CRDB.
Akieleza namna alivyoshinda gari hilo, Ojweke amesema muamala wa mwisho alioufanya kwa kutumia programu ya Simbanking ni kutuma fedha kwa mtu aliyemuomba msaada kutokana na changamoto alizonazo.
“Kuna mama mmoja alinitumia ujumbe mfupi wa simu akiniomba msaada. Yeye ni mjane, alinieleza walilala bila kula na wameamka hawana uhakika wa chakula. Nilimtumia hela kidogo kupitia Simbanking. Muda mfupi baada ya kumtumia hela hiyo ndio nikapokea simu kutoka Benki ya CRDB wakinieleza nimeshinda gari kutokana na matumizi ya Simbanking. Nilistaajabu ila nilifurahi pia,” amesema Ojweke.
Ojweke amesema amekuwa akitumia programu ya Simbanking kwa muda mrefu kwani ni rahisi na ina ufanisi mkubwa tofauti na programu za benki nyingine.
“Namshukuru mwajiri wangu anayenilipa mshahara ulioniwezesha kupata zawadi hii. Kwa wateja wenzangu wa Benki ya CRDB, tumieni Simbanking ili mshinde fedha taslimu, simu za mkononi hata gari kama nilivyoshinda mimi. Kuna gari kubwa la Vanguard, msipoitumia fursa, naweza nikashinda tena,” amesema Ojweke.
Mshindi huyo ambaye amekuwa mteja wa Benki ya CRDB tangu mwaka 2001, amekabidhiwa gari hilo lenye thamani ya Sh.Milioni 20 lililokatiwa bima kubwa na kujaziwa mafuta ‘full tank.’
Akikabidhi zawadi hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili amesema maendeleo ya sayansi na teknolojia yameulazimu ulimwengu kuhamia kwenye uchumi wa kidijiti hivyo Tanzania nayo haipaswi kubaki nyuma ndio maana wanahamasisha matumizi ya Simbanking, jukwaa lililoboresha linalokidhi mahitaji ya mteja kwa wakati.
“Leo tunamtangaza kaka yangu Jared kuwa mshindi wa gari. Yeye ni ni mshindi wa pili baada ya Mayani Yahaya Hassan wa mkoani Dodoma kushinda miezi miwili iliyopita. Simbanking ni ya kila mtu, unaweza kumaliza mahitaji yako ukiwa mahali popote,” amesema Adili.
Ikiwa benki kiongozi nchini, Adili amesema Benki ya CRDB inahakikisha wakati wote inaboresha huduma zake ili kukidhi mahitaji ya wateja ikitambua kwamba matarajio yao yanabadilika kila siku.
Balozi wa Simbanking, Priva Shayo almaarufu kama ‘Privaldinho’ amesema kwa maisha ya sasa gari ni nyenzo muhimu ya kurahisisha shughuli za mtu hasa mjini ambako watu wanakimbizana na ratiba.
“Kama lilivyo gari, huduma za Simbanking nazo ni muhimu kwani unaweza kununua muda wa maongezi, kununua luku au kulipia bili za maji na huduma nyingine. Mshindi wa leo anakuwa amekamilisha mahitaji muhimu kwa maisha ya mjini, watoto wake hata ndugu na marafiki nao watahamasika kutumia huduma za Simbanking,” amesema Privaldinho ambaye ni meneja mawasiliano wa Klabu ya Yanga.
Kampeni ya Benki ni SimBanking ilizinduliwa mapema Februari na itadumu mpaka Desemba na kumpa kila amteja anayefanya miamala kwa Simbanking kushinda moja kati ya zawadi kemkem zinazoendelea kutolewa kila siku kabla mshindi wa jumla atakayeondoka na gari aina ya Vanguard hajahitimisha mchuano huu.
Katika kipindi cha kampeni hii, matumizi ya huduma za Simbanking sambamba na idadi ya wateja wanaojisajili kwenye jukwaa hili la kidijiti yameongezeka na hadi Desemba kutakuwa na namba kubwa zaidi.