NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAFANYAKAZI wa Benki ya Exim Tanzania, wateja pamoja na wadau wengine katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Mtwara jana walijotokeza kwa wingi kwenye matawi ya benki hiyo pamoja na maeneo maalum yaliyoandaliwa na benki hiyo ili kuchangia damu ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Uchangiaji Damu duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati zoezi hilo likiendelea, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Stanley Kafu alisema hatua hiyo ni mwendelezo tu kwa kuwa wamekuwa wakifanya hivyo tangu mwaka 2010 na lengo kuu likiwa ni kukabiliana na tatizo upungufu wa damu salama kwenye vituo vya afya hapa nchini.
“Mara zote tumekuwa tukijisikia kuwa na wajibu mkubwa kama benki ya kizalendo kila tunapolekea maadhimisho muhimu haya ya uchangiaji damu kwa kuwa tunaamini kwamba tunapata fursa ya kutimiza wajibu wetu kama sehemu ya jamii lakini pia kwa kufanya hivyo tunakuwa tumeshiriki kuokoa maisha ya wenzetu wakiwemo wakina mama, watoto na wahanga wa ajali wanaopoteza maisha kwa kukosa damu salama pale wanapoihitaji,’’ alisema.
Kauli hiyo ya Kafu inakwenda sambamba na kauli mbiu ya uchangiaji damu ya mwaka huu inayosema: “Changia Damu, Changia Mazao ya Damu (Plasma), Changia mara kwa mara’’. Kauli mbiu hiyo inalenga kuonyesha namna gani maisha ya watu wenye uhitaji wa damu huokolewa na wenzao wanaojitokeza kuchangia damu mara kwa mara.
“Kufuatia mafanikio makubwa na uungwaji mkono tunaoupata kupitia kampeni hii Benki ya Exim tunawashukuru sana wafanyakazi wa benki kwa namna wanavyojitolea kuchangia damu kila linapofanyika zoezi hili. Shukrani hizi pia tunazielekeza kwa wateja wetu na wadau wengine ambao waliojumuika nasi leo katika mikoa mitano tunayoendesha zoezi hili. Ushirikiano huu baina yetu na wadau wetu unathibitisha uhusiano imara kati ya benki na jamii tunaihudumia ambao kimsingi unakwenda nje ya mipaka ya biashara hadi kwenye hatma ya maisha yetu.’’ alisema.
Akizungumza wakati akisimamia zoezi hilo Offisa Uhamasishaji na elimu kwa umma kutoka Mpango wa taifa wa damu salama (NBTS) Marry Meshy alisema uhaba wa damu hapa nchini umekuwa ukichangiwa kwa kiasi kikubwa na mtazamo wa Wananchi walio wengi kwamba wapo tayari kuchangia damu pale tu inapohitajiwa na mmoja wa wanandugu wa familia husika.
Nao baadhi ya wadau walioshiriki zoezi hili zikiwemo taasisi za kijamii walisema wamekuwa wakiguswa na hitaji hilo muhimu la kuchangia damu kila mwaka kwa kuwa wao ni sehemu ya jamii na wanahitaji kuleta mabadiliko ndani ya jamii kwa kuokoa maisha ya wenzao wenye uhitaji wa huduma hiyo muhimu.