NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba amepokea gawio kubwa zaidi kupata kutolewa na taasisi ya kifedha la shilingi bilioni 45.8 linalotokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya Benki ya CRDB kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dk Ally Laay.

Makabidhiano hayo ya hundi kifani yalifanyika katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Natu Mwamba pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi na mashirika ya umma yenye hisa ndani ya Benki ya CRDB.
Akizungumza katika hafla hiyo Juni 9, 2023 Waziri wa Fedha aliipongeza Benki hiyo kwa kutoa gawio kwa Serikali.
Dk Nchemba aliipongeza Benki ya CRDB kwa kupata matokeo mazuri ya fedha mwaka 2022 ambayo yamepelekea kuongezeka kwa gawio kwa wanahisa ikiwamo Serikali.
“Ongezeko hili la gawio ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa Benki yetu ya CRDB inazidi kuimarika zaidi kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea na jambo linalowapa moyo Watanzania na wawekezaji kuwa benki inatoa huduma bora katika jamii”, amesema Dk Nchemba.
Dk Nchemba amesema fedha zilizopatikana kupitia gawio hilo zitakwenda kusaidia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeianisha katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2023/2024.
“Kipekee kabisa niipongeze Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB kwa kazi nzuri mnayoifanya,” ameongezea Dk Nchemba.
Ameipongeza Benki ya CRDB kwa kukamilisha mkakati wa muda wa wakati wa 2018/2022 kwa mafanikio makubwa ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita faida ya benki hiyo imekua kwa asilimia 875.
“Niwapongeze pia kwa matokeo ya fedha ya robo ya kwanza ya mwaka huu ambapo Benki yetu hii imepata faida baada ya kodi ya Sh. Bilioni 90, mkiendelea na kasi hii mwakani tunategemea kupata gawio nono zaidi,” amesema Dk. Nchemba.
Akielezea namna ambavyo Serikali inaridhishwa na umahiri wa Benki ya CRDB katika kufanya biashara kiushindani, Dk. Nchemba aliipongeza Benki hiyo kwa kupanua wigo wake kwa kuanzisha kampuni tanzu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kampuni tanzu ya CRDB Insurance Co. Ltd, pamoja na taasisi ya CRDB Bank Foundation ambayo imeonyesha kuwa mstari wa mbele katika kuchochea ujumuishi wa kiuchumi kupitia programu ya IMBEJU.
Dk Nchemba amezitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa Benki ya CRDB katika kuleta faida kwa Serikali na Wanahisa kutokana na Uwekezaji.
Alizitaka Taasisi na Mashirika yote ambayo Serikali ina hisa kuweka mikakati madhubuti itakayoleta tija, huku akiwataka viongozi ambao taasisi zao zimeendelea kuwa na matokeo mabovu kujitathmini kiutendaji.
Aidha, Dk Nchemba aliihakikishia Benki ya CRDB na wadau wengine wa maendeleo nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha na kuweka mazingira rafiki na endelevu ya kufanya biashara katika sekta ya fedha na sekta nyinginezo ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje.
Dk Nchemba amesema Serikali ina mpango wa kuja na programu kabambe ambayo itasaidia kuboresha sekta binafsi na kupunguza mikopo chechefu nchini.
Pia amesisitiza juu ya weledi wa wafanyakazi wa mabenki katika utoaji wa mikopo kwa kuhakikisha fedha zinazokopeshwa zinakwenda kwenye miradi au biashara endelevu.
Naye katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Mwamba aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Benki ya CRDB kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kusimamia benki hiyo na kupelekea matokeo mazuri ya kifedha na kukua kwa gawio kwa wanahisa ikiwamo Serikali.
Dk Mwamba aliipongeza pia Benki Kuu kwa usimamizi mzuri wa sekta hiyo ambayo imechangia katika utendaji mzuri wa taasisi za kifedha, na uwepo wa huduma bora na nafuu kwa wananchi.
Akikabidhi gawio Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dk. Laay alisema kuwa gawio hilo ni sehemu ya faida ya Sh.Bilioni 351.4 baada ya kodi ambayo Benki hiyo imeipata katika mwaka wa fedha 2022.
“Katika Mkutano wa Wanahisa uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) Mei mwaka huu, Wanahisa wa Benki ya CRDB walipitisha kwa pamoja gawio la Sh.45 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 25 na hivyo kufanya jumla ya gawio la mwaka huu kufikia Sh.Bilioni 117.5,” amesema Dk.Laay.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kukua kwa thamani ya uwekezaji wa wanahisa wa benki hiyo kutokana na mafanikio ambayo benki hiyo imeyapata katika utekelezaji wa mkakati wake wa biashara wa muda wa kati wa mwaka 2018 – 2022.
Nsekela amesema katika kipindi hicho Benki ya CRDB imepata mafanikio makubwa ya kiutendaji yaliyopelekea benki hiyo kuwa na mchango mkubwa katika kusaidia jitihada za maendeleo nchini.
Nsekela amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita benki hiyo imelipa jumla ya kodi ya Sh.Trilioni 1.1 kwa serikali.
“Katika kipindi cha miaka mitano pia tumeweza kuongeza ajira zaidi ya 600 nchini, tukitumia zaidi ya Sh.Trilioni 1.3 kulipa mishahara na marupurupu, tumefanya kazi na wazabuni zaidi ya 1,000 na kulipa zaidi Sh.Bilioni 625,” amesema Nsekela huku akibainisha benki hiyo imetumia zaidi ya Sh.Bilioni 14 katika miradi ya kijamii kupitia sera yake ya uwekezaji kwa jamii.
Nsekela alimweleza Dk Nchemba kuwa mwaka huu utekelezaji wa mkakati wetu mpya wa biashara wa muda wa kati wa miaka mitano (2023 – 2027) ambao unasisitiza katika ‘Mageuzi Thabiti’.
Kupitia mkakati huo Benki ya CRDB imejipanga kikamilifu katika kuwekeza kwenye ubunifu wa huduma, bidhaa, na programu zitakazosaidia kuboresha maisha ya watu na uchumi wa Taifa kwa ujumla wake.
Pamoja na kukabidhi gawio kwa Serikali kuu kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA, Benki ya CRDB pia imekabidhi gawio kwa taasisi na mashirika mbalimbali ya Serikali ikiwamo PSSSF, NSSF, ZSSF, NHIF, Local Government Loans Board, Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Umoja Unit Trust Scheme, pamoja na Halmashauri Mbinga, Shinyanga, Mufindi, Chunya na Rungwe.
Akipokea gawio kutokana na uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vina na Walemavu, Patrobas Katambi alizihimiza taasisi nyigine za umma nchini kuwekeza katika hisa ili kupanua wigo wa mapato katika taasisi zao.
Serikali ndio mwanahisa mkubwa ndani ya Benki ya CRDB kutokana na kuwa na umiliki wa asilimia 21 kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA kushirikiana na Serikali ya Denmark, huku taasisi na mashirika ya umma yakiwa na umiliki wa hisa za asilimia 15.
–