*Yaahidi Uwekezaji zaidi kwenye Ligi
NA MWANDISHI WETU, MBEYA
MDHAMINI Mkuu wa Ligi ya Soka ya Tanzania Bara, NBC Premier League, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeipongeza Klabu ya Yanga SC kwa kuibuka na ubingwa wa ligi hiyo Msimu 2022/2023 huku ikiahidi kuendelea kuboresha zaidi udhamini wake kwenye ligi hiyo.
Benki hiyo imeahidi kuendelea kuongeza ‘motisha’ zaidi kwenye ligi hiyo sambamba na kubuni huduma mbalimbali za kibenki zinazolenga kuwasaidia wachezaji na wadau wengine wa mchezo huo ili kuwajengea uwezo wao pamoja vilabu vyao.
Hatua hiyo inatajwa kuwa inalenga kuipa hadhi zaidi ligi hiyo ili iendelee kuwa bora kwenye orodha ya ligi bora barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi kombe kwa Bingwa wa ligi hiyo timu ya Yanga SC iliyofanyika baada ya kukamilika kwa mchezo kati timu za Yanga na Prisons jijini Mbeya iliyofanyika jijini hapa mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi wa Fedha wa NBC Barnabas Waziri aliahidi kuwa benki hiyo itaendelea kuwa mdhamini mkuu wa ligi hiyo na pia itaendelea kutoa mchango katika sekta ya michezo kwa upana wake. Katika mchezo huo timu ya Yanga SC iliibuka na ushindi wa 2 – 0
“Katika msimu huu wa 2022/2023 benki ya NBC tulifanya maboresho kadhaa ikiwemo kubuni huduma mbalimbali za kibenki zinazowalenga wachezaaji na wadau wa ligi hii ikiwemo utoaji huduma bima kwa wachezaji wa ligi hii pamoja na familia zao pamoja na mikopo ya mabasi kwa vilabu vinavyoshiriki ligi.
“Pia tulikuwa tukitoa zawadi kwa wachezaji bora pamoja na kocha bora wa kila mwezi lengo likiwa ni kuongeza motisha na kuchochea ushindani,’’ amebainisha.
Zaidi Waziri ameipongeza timu ya Yanga FC pamoja na mashabiki wake kwa ubingwa huo hasa kwa kwa kuwa ligi hiyo ilikuwa ngumu na yenye ushindani kutokana na ukweli kuwa kila timu iliyoshiriki ligi hiyo ilikuwa imefanya maandalizi ya kutosha bila changamoto za kiuchumi kufuatia udhamini mnono uliofanywa na benki hiyo pamoja na wadhamini wengine.
“Udhamini wa NBC pamoja na wadau wengine kwenye ligi hii umesaidia sana kutatua changamoto kadhaa zilizokuwa zinapunguza ushindani kwenye ligi ikiwemo changamoto za kifedha, usafiri duni kwa baadhi ya timu na ukosefu wa huduma za afya ikiwemo bima za afya.
” Hatua hii imeongeza ushindani kwenye ligi na hiyo ndio sababu tunawapongeza sana Yanga FC kwa kuibuka washindi kwenye ligi hii ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa,’’ amepongeza.
Akikabidhi kombe hilo kwa Yanga SC, huku akishuhudiwa na maelfu ya mashabiki wapenda soka wa jiji la Mbeya na mikoa jirani ya Nyanda za Juu Kusini, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera aliishukuru benki ya NBC kuwa mdhamini mkuu wa ligi hiyo huku akibainisha kuwa udhamini wa benki hiyo umekuwa na matokeo chanya kwa soka la Tanzania.
“Udhamini wa NBC umewezesha kuongeza ushindani kwenye ligi na kuboresha soka letu. Leo hii tunajivunia kuwa na ligi bora barani Afrika tukishikilia nafasi ya tano. Naipongeza sana benki ya NBC kwa kufanya mambo makubwa katika ligi na soka la nchi yetu kwa ujumla,” alipongeza Homera.
Pia Mkuu huyo wa mkoa aliipongeza timu ya Yanga FC kwa kutwaa ubingwa huo huku akibainisha kuwa haikuwa rahisi kwa timu hiyo kuibuka kinara wa ligi hiyo kutokana na ushindani mkali kutoka kwa timu pinzani.
