NA MWANDISHI WETU, MWANZA
JAJI Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapha Siyani amefungua semina kwa njia ya e-Mikutano ukioandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF kwa Majaji na Mahakimu wa Kanda ya Ziwa, Tabora, Manyara na Kigoma waliokutana jijini Mwanza.
Semina hiyo ni ya siku mbili kuanzia Juni 9 hadi 10 , 2023.
Amesema kupitia semina hiyo NSSF imefungua njia ambayo wadau wengi wataifuata, hivyo Mahakama na NSSF kama ilivyo kwa taasisi nyingine zinazotoa huduma kwa jamii haziwezi kufanikiwa ikiwa kila taasisi itajifungia ikiamini inaweza.
“Niwahakikishie wadau wetu wote wakiwemo NSSF kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kuwashirikisha katika mipango yake na hususan inapotekeleza mpango mkakati wake wa miaka mitano utakaokamilika ifikapo mwaka 2025,” amesema.
Jaji Kiongozi Siyani amesema masuala ya hifadhi ya jamii ni mambo yanayohusu maisha ya watu wakiwa hai au baada ya kuondoka duniani na kuwa malipo ya watu hao hasa yanapohusisha mirathi yamekuwa na changamoto ambapo moja ya mambo yanayoweza kuondoa changamoto hizo ni mawasiliano kati ya Mahakama na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Naye, Rais wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), Jaji John Kahyoza ameushukuru uongozi wa NSSF kwa kuwawezesha kushiriki semina hiyo ambayo ni moja ya utekelezaji wa malengo makuu ya chama hicho ambacho lengo lake ni kulinda uhuru wa Mahakama na kujenga ujuzi kwa Waheshimiwa Majaji na Mahakimu Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani, Godfrey Ngonyani, amesema ushirikiano baina ya Mfuko na mhimili huo ni muhimu na ni sehemu ya mkakati wa NSSF kuendelea kushirikiana na wadau, ikiwemo kuandaa vikao na semina.
Ngonyani amesema Mfuko umekuwa ukishirikiana na Mahakama kupitia ziara ambazo zilifanywa Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini na zinatarajiwa kuendelea katika kanda nyingine na kuwa Mahakama ni wadau muhimu kwenye mashauri dhidi ya waajiri wanaokiuka sheria kwa kushindwa kuwasilisha michango kwa wakati.


Mkutano wa Siku ya kwanza na ya pili ukiendelea








Matukio mbalimbali katika picha