NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC ) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wamezindua mpango rasmi wa ufadhili wa masomo ya ufundi stadi kwa vijana, kupitia Mamlaka za Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini yaani VETA.
Mpango huu maalum ujulikanao kama “NBC Wajibika Scholarships” utalenga kutoa ufadhili kwa wanafunzi 1,000 katika vituo mbalimbali vya VETA hapa nchini.
Akizungumza jijini Dar es salaam Juni 9, 2023 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi amesema Benki ya NBC imetenga kiasi cha Sh.Milioni 100 kushamirisha ufadhili huo. Masomo mbalimbali ya ufundi ikiwemo ushonaji, userelema, ufundi magari, ujenzi, Upambaji na mengineyo, yanufaika na mpango huu maalumu.
Amesema zaidi ya ufadhili wa masomo, Benki pia itawaingiza vijana hao 1,000 katika mpango maalum wa elimu ya fedha ujulikanao kama “NBC Business Club” na kuwafungulia akaunti maalum za “NBC-KUA Nasi” zitakazowapa wasaa wa kutunza fedha bila gharama, kupata ushauri juu ya uwekezaji na kuwapa fursa za uwezeshaji kiuchumi kupitia mikopo ya kujiendeleza kibiashara.
“Benki ya NBC inaendelea kusisitiza dhamira yake ya kuwa mdau mkubwa wa elimu na uwezeshaji kwa vijana kwani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, imewekeza zaidi ya shilingi 350 milioni katika kutoa ufadhili wa masomo kwa vijana 70 katika Vyuo mbalimbali vya elimu ya juu nchini”amesema
Kwa upande wake Waziri Elimu, Sayansi na Taknolojia Prof.Adolf Mkenda ameipongeza Benki ya NBC kwa hatua ambayo wameifanya hasa kuhakikisha vijana ambao watapata fursa ya ufadhili huo watawapa nafasi ya kujifunza masuala ya fedha hasa kwenye masuala ya ujasiriamali na kuweza kujitegemea.
Amesema kuna umuhimu mkubwa Vyuo vyote vya Ufundi na Vyuo vya Amali nchini vikasaidia kupata idadi kubwa ya watu wenye uwezo wa kuzalisha vitu kama nguo, viatu na vitu vingine ambavyo vitasaidia kuongeza ajira hapa nchini kulinda fedha zetu za kigeni.
Aidha ametoa wito kwa wadau wengine waweze kujitokeza na kuungana na Wizara katika kuhakikisha vijana wengi wanaojiunga na VETA waweze kupata ufadhiri wa masomo.
Amesema Serikali inaangalia namna ya kuboresha mafunzo katika VETA ili kuhakikisha vijana wanaohitimu wanakuwa na ujuzi mkubwa ambao utapelekea kujiajiri ama kuajiriwa kwa haraka zaidi kupitia mafunzo ambayo wamesomea.
Pamoja na hayo amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa VETA kwa ngazi za Wilaya nchini ambapo mpaka sasa wanaendelea naujenzi wa VETA 64 kwa mkupuo nchi nzima na mpaka sasa Mkoa mmoja ndo umebaki hauna VETA ya Mkoa.
Makubaliano rasmi pamoja na kusaini makubaliano hayo yatafanyika Juni 28 kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia pamoja na Benki ya NBC ambao watakabidhi fedha kwaajili ya kutoa ufadhili.