DAR ES SALAAM, TANZANIA
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeionya Serikali ya Tanzania kutoruhusu Bandari za Tanzania kubinafsishwa kwa Serikali ya Dubai kama ambavyo nyaraka mbalimbali zilizoenea kwenye mitandao ya jamii zinavyosomeka.
Chadema kupitia kwa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kimesema kama Serikali itaingia kwenye mkataba huo basi chama chake kitawaamsha Watanzania ili waikomboe nchi yao.
Akizungumza kutoka nchini Italia, Mbowe amesema chama chale kinashangaa kwanini bandari zinazotaka kubinafsishwa ni za Tanzania Bara pekee bila kuzihusisha bandari za Zanzibar.
Napenda kusema hili na nisieleweke vibaya lakini kama viongozi ni lazima tuambiane ukweli. Rais Samia ni Mzanzibari, Waziri wa mambo ya Uchukuzi ambaye bandari zipo chini yake, Makame Mbarawa ni Mzanzibari wawili hawa wanatufanya tufikirie kuwa wana mkakati wa kuuza mali za Tanganyika kwa maslahi yao binafsi,” alisema Mbowe
Mwenyekiti huyo alisema mkataba huo ni hatari kwa usalama na uhuru wa Watanzania kwani pamoja na kutaka muwekezaji akabidhiwe bandari zote za bahari na maziwa makubwa kwa mkataba usiokuwa na kikomo lakini pia unaelekeza muwekezaji apewe ardhi ya ukubwa wowote anaoutaka bila kumkatalia.
Huu ni mkataba wa aina gani ambao hausemi muwekezaji anawekeza fedha kiasi gani, pesa kiasi gani serikali itapata kwa muda gani na mkataba unataka serikali imiliki gati moja tu ya abiria? Chadema tunaitaka Serikali kuachana na mradi huo na Bunge likatae kupitisha azimio hili kama serikali halitaliondoa vinginevyo tutawanyanyua wananchi.” aliongeza Mbowe
Mbowe amesema kwa hapa tulipofika, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Waziri wa uchukuzi wajitafakari kuona kama wanapaswa kuendelea na nyadhifa zao