DENIS CHAMBI, TANGA
MIRADI saba yenye thamani ya Sh. Billioni 2.7 inatarajiwa kuzinduliwa na mbio za mwenge wa Uhuru ndani ya Halmashauri ya jiji la Tanga Juni 9, 2023
Akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari leo Juni 6, 2023 Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashimu Mgandilwa amesema kuwa mwenge huo ambao utapokelewa kwenye uwanja wa ndege wa Tanga ukitokea Pemba utaipitia miradi yote iliyotekelezwa ndani ya halmashauri hiyo ambapo mara baada ya kuzitembelea wilaya zote nane na Halmashauri 11 utaelekea mkoa wa Kilimanjaro.
Mgandilwa amesema kuwa miradi hiyo ni uzinduzi wa madarasa mawili katika shule ya msingi Mnyanjani, ufunguzi wa jengo linalohudumia wagonjwa wa nje lililopo katika hospital ya Safi Medics, uzinduzi wa barabara ya Askari na Lumumba iliyojengwa kupitia fedha za mapato ya ndani, zoezi la upandaji wa miti katika eneo la Mabayani ikiwa inaendana sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu utunzaji wa mazingira.
Miradi hiyo itakayozinduliwa ni pamoja na mradi wa uwezeshaji wa vijana ambayo inatekelezwa na serikali katika kuwawezesha vijana kuweza kujiajiri wenyewe kupitia kilimo na ufugaji, mradi wa maji uliofadhiliwa na taasisi ya Islamic help katika eneo la Mwahako, mradi wa kitega uchumi wa sheli uliojengwa na moja ya wadau wa Halmashauri hiyo.
“Serikali ya Rais Samia inaendelea kuboresha miundombinu katika sekta ya elimu ambapo kwenye mbio za mwenge tutapata fursa ya kwenda Mnyanjani na tutafanya ufunguzi wa madarasa mawili ya shule ya msingi Mnyanjani, tutakwenda katika hospital ya Safi Medics kuzindua jengo la wagonjwa wa nje , (OPD) pamoja miradi ambayo tutapata fursa ya kuzinduliwa na mwenge wa Uhuru ina thamani ya Sh.Billioni 2.7” amesema Mgandilwa na kuongeza
Pia Mgandilwa alieleza kuwa kutakuwa na mradi wa sekta ya barabara ambapo barabara ya Askari na Lumumba iliyojengwa kwa fedha za mapato ya ndani uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali kwahiyo mwenge wa Uhuru utakwenda kwaajili ya uwekezaji wa jiwe la msingi uboreshaji wa barabara ya lami ambayo inajengwa
“Kama tunavyofahamu malengo ya mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka huu 2023 ni masuala mazima ya mazingira kwahiyo tutakwenda eneo la Mabayani kushuhudia zoezi zima la utunzaji wa mazingira na baada ya hapo mwenge wa uhuru utakesha katika eneo la viwanja vya Mwamboni” amesema Mgandilwa.