NA MWANDISHI MAALUMU, DAR ES SALAAM
HOSPITALI ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia imemtuma daktari wa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kuongeza ujuzi wa upasuaji wa moyo.
Hospitali hiyo itaanza kutoa huduma za upasuaji wa moyo hivi karibuni hivyo inaandaa mkakati wa utekelezaji.
Hayo yamesemwa leo Juni Mosi, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk.Peter Kisenge wakati akizunguma na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Dk Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema daktari huyo amekuja nchini kujifunza jinsi ya kuanza kutoa huduma ya upasuaji wa moyo pamoja na kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkurugenzi huyo Mtendaji alisema daktari huyo anajifunza vitu vya muhimu vinavyotakiwa kuwepo katika Hospitali kabla ya kuanza kutolewa kwa huduma ya upasuaji.
“Mwezi wa nne tulisaini mkataba na Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia wa kuwatibu wagonjwa wa moyo na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa kuwatibu wagonjwa hao”.
“Katika kuhakikisha Hospitali hii inaanza kutoa huduma za upasuaji wa moyo wiki ijayo madaktari wetu watatu ambao ni wa usingizi, wagonjwa wa dharura na mahututi na upasuaji watakwenda nchini Zambia kuona ni jinsi gani tutawajengea uwezo katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo ili waanze kutoa huduma hiyo”, alisema Dk.Kisenge.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau alisema daktari huyo amekuja kujifunza jinsi atakavyoweza kufanya upasuaji wa moyo katika nchi yenye rasilimali chache.
Dk. Sharau alisema amefurahi kukutana na daktari ambaye ametoka katika mafunzo hivi karibuni nchini Israeli mahali ambapo yeye pia alipata mafunzo miaka kumi iliyopita na hii imemfanya kukaa naye kwa ukaribu na kufanya kwa pamoja yale waliyojifunza katika upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto.
“Ni mara yangu ya kwanza kukutana na daktari huyu tumefanya kazi pamoja na tumebadilishana mawazo ,pia nimemweleza changamoto tulizokutana nazo katika kuanzisha upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto na njia ambazo tulitumia kutatua changamoto hizo ili kujijenga katika upasuji huu wa moyo”.
“Naamini kwa ushirikiano huu tutawainua na wao kuanzisha huduma ya upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto ili watoto walioko nchini Zambia wenye matatizo ya moyo wapate matibabu kwa karibu”, alisema
Aidha aliushukuru uongozi wa Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) lililoko nchini Israel kwa kuwa sehemu ya kuwajengea uwezo wataalam wa afya kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Naye daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia Ziwa Mudaniso alisema amekuwa na muda mzuri wa kujifunza kwa madaktari wa JKCI katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto.
“Nimefika JKCI kwa ajili ya kujifunza namna madakltari hawa wanavyofanya kazi na ninaahidi kufanya haya pindi nitakaporudi Zambia, kutumia vifaa tiba vilivyopo kuwahudumia watoto wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo”, alisema Dk Mudaniso
Daktari huyo yupo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa muda wa wiki moja kwaajili ya kujengewa uwezo baada ya kumaliza mafunzo ya upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Wolfson iliyopo nchini Israel kupitia ufadhili ya Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH).