NA MWANDISHI WETU, TABORA
SAKATA la watoto mapacha waliozaliwa kabla ya muda katika Kituo cha Afya Kaliua mkoani Tabora na kuzua taharuki baada ya pacha mmoja kunyofolewa jicho moja na ngozi ya paji la uso limemalizika baada ya kuzikwa rasmi nyumbani kwao Kitongoji cha Mwangaza cha Kalemela, Kata ya Muungano wilayani Urambo baada ya familia kuridhika na hatua zilizochukuliwa na serikali.
Akizungumza baada ya mazishi hayo baba wa watoto hao, Isaka Raphael aliiomba serikali isimamie hatua iliyobaki kwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa na kuhakikisha haki inatendeka kwa kuwapata wahusika wengine walioshirikiana na wauguzi hao.
“Serikali isiishie kwa wauguzi hao pekee bali ifuate mnyororo wa wanufaika wengine wa uovu uliofanywa dhidi ya wanangu na hiyo itasaidia kukomesha kabisa matukio kama hayo siku za usoni,” alisema.
Baba yake mzazi na Isaka Rafael, Macho Maulid na baba yake mdogo, Alex Paulo waliishukuru serikali hususani ofisi ya mkuu wa wilaya kwa ushirikiano waliouonesha katika kipindi chote cha mkasa huo mpaka hatua ya mazishi.
“Tangu siku ya kwanza tulipoenda katika ofisi yake ameambatana nasi tukaenda mpaka kituo cha afya na baadaye akaja nyumbani mara mbili, tatu na mpaka leo tuko naye hapa katika mazishi, tunaomba asichoke achukue hatua kali kwa waliohusika na watumishi wengine wanaodharau wananchi masikini,” alisema Paulo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dk Rashid Chuachua aliyehudhuria msiba huo aliwataka wananchi wa Kaliua wasipoteze imani ya huduma za afya wilayani humo kwa sababu ya tukio hilo kwa kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua kuhakikisha usalama wa wananchi wake.
“Nitoe wito kwa wananchi wa Kaliua kwamba tukio hili limetokea katika kituo chetu cha afya lisiwakatishe tamaa kwamba huduma za afya kwenye Wilaya ya Kaliua zina changamoto, ninachotaka kusema ni kwamba serikali imejipanga vizuri na itachukua hatua wakati wowote na katika sekta yoyote pale ambapo linatokea jambo ambalo sio la kawaida serikali itachukua hatua na itaendelea kulinda maslahi ya wananchi,” alisema.
Mazishi hayo yamefanyika siku 15 tangu tukio hilo kutokea na hii ni baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian kusema kwamba uchunguzi umekamilika na wauguzi wanne watafikishwa mahakamani