NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KATIKA kuhakikisha wanaokoa maisha ya mama na mtoto wilayani Korogwe, Shirika la Lions Clubs International limetoa msaada wa Jenereta ya 10KVA, Viti sita vya Magurudumu na Mashine sita za kidijitali za kupima Presha.
Msaada huo ambao umegharimu sh. Milioni 10 umetolewa kwa kushirikiana na Arun wa Specialised Engineering (T) Ltd, Ukumbi wa Tarangini, Lions Club of DSM Incredibles na Lions Club of DSM Tanzanites utakwenda kwenye wodi ya watoto wachanga katika Hospitali ya Korogwe.
Akipokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo amewashukuru kwa kuguswa katika kuwasaidia watoto na kina mama.
“Msaada huu utakwenda kusaidia serikali ambayo imejikita katika kuboresha huduma za afya. Hii iliyofanyika inakwenda kuongeza kasi zaidi ambayo tayari serikali imeanza,” amesema Jokate.
Awali akizungumza katika makabidhiano hayo kwa niaba ya Kiongozi wa kanda ya Tanzania, Lion Mustansir Gulamhussein, Katibu wa Kabineti Bhavika Sajan, amesema dira na malengo yao ni kurudisha kwa jamii inayowazunguka, ambapo huduma zao zimejikita katika maeneo kama vile Mazingira, Kupambana na njaa, Kisukari, Macho pamoja na Saratani kwa Watoto.
“Tunasema kua kila kwenye uhitaji basi Lions tupo na Kadri tunavyokua pamoja ndivyo tunavyotoa huduma nyingi zaidi.
Mchango wetu kwa leo ni Jenereta ya 10KVA, Viti sita vya Magurudumu na Mashine sita za kidijitali za kupima Presha. Tunatarajia kuendelea kushirikiana zaidi na Wodi hii ya watoto katika siku zijazo,” amesema.
Ameongeza kuwa Lions Clubs International imegawanyika katika maeneo kadhaa duniani huku ikiwa na wanachama wapatao milioni moja nukta nne kwa Afrika, ambapo Tanzania ipo katika ukanda wa 411 ikiwa ni sehemu ya kanda jumuishi ambapo inahusisha nchi jirani kama Kenya, Uganda, Ethiopia na Visiwa vya Shelisheli.
“Tanzania inafahamika kama kanda 411 C ikiwa na klabu takribani Ishirini na Nne na wanachama Mia Sita Ishirini mpaka sasa.
Kazi za Lions zinaanzia kwenye jamii na kila jamii ina mahitaji yake muhimu. Licha ya kua tunatoa huduma katika njia nyingi juhudi zetu tumezikita katika maeneo makuu matano ili kuigusa zaidi jamii,” amesema.