NA MWANDISHI WETU, GEITA
DAUDI Lufungulo (30) amepoteza maisha baada ya kuzama majini wakati akioga kwenye bwawa la maji lililopo eneo la Mtaa wa Samina, Kata ya Nyankumbu mjini Geita.
Mkuu wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji wilayani Geita, Wambura Fidelis alithibitisha tukio hilo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Samina mara baada ya kuokoa mwili wa marehemu.
Wambura alisema uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha ajali hiyo ni kina kirefu na wingi wa tope wa bwawa hilo ambalo marehemu alienda kuoga na kujikuta amezama.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Samina, Joseph Kazungu alisema marehemu alikuwa ni mtu ambaye si mwenyeji sana eneo hilo kwani hana muda mrefu tangu amehamia Mtaa wa Samina.
“Ukiangalia marehemu ni mtu ambaye amekuja hivi karibuni, inawezekana hakujua kina cha hili dimbwi, amekuwa labda akiliona na kuogelea hakujua kina chake kipo vipi,” alisisitiza Kazungu.
Shuhuda wa tukio hilo, Golani Simon alisema marehemu aliwakuta eneo hilo wakiwa wanafua na aliwaomba sabuni ili aoge na alipopewa sabuni alivua nguo na kujirusha kwenye maji kisha kuzama.
Shemeji wa marehemu, Joel Daudi alisema kabla ya umauti walimualika marehemu waende kuoga naye kwenye dimbwi hilo naye aligoma na kuwaarifu hakuwa tayari kwenda kuoga muda huo