Na Mwandishi wetu
KATIKA kuelekea wiki ya maadhimisho ya siku ya walinda amani duniani, Kikosi cha sita cha walinda amani kutoka Tanzania (TANBAT 6) kimeadhimisha kwa kurekebisha miundombinu ya barabara iliyoharibika vibaya maeneo ya Beriberati mkoani Mambele Kadei huko Afrika ya Kati.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa Habari wa kikosi hicho, Kapteni Mwijage Inyoma alisema kikosi hicho kinachohudumu chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) kimeanza shughuli hizo kuelekea kilele cha siku ya walinda amani duniani itakayofanyika Mei 29, 2023.
Alisema mbali na shughuli hizo, walinda amani hao watafanya doria na kuhakikisha kunakuwepo na usalama katika maeneo yote ya Afrika ya kati hasa mkoa wa Mambele Kadei.
“Kazi kubwa ya kikosi hiki ni kuhakikisha usalama , lakini shughuli za maendeleo ni moja ya majukumu muhimu ambayo wanapaswa kufanya hivyo hichi wanachokifanya kitachangia kwa kiasi kikubwa kudumisha amani na usalama kwa kuwa mambo haya yanayofanyika yanaishirikisha jamii na viongozi wao kwa ujumla,” alisema Kapteni Inyoma
Naye kamanda wa TANBAT 6, Luteni Kanali Amini Mshana alisema ingawa jukumu lao kubwa ni ulinzi wa raia lakini kufanya shughuli za maendeleo kumewasogeza walinda amani karibu na wananchi na kusaidia kwa kiasi kikubwa operesheni zao.
Siku ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa (UN) uhadhimishwa kila mwaka Mei 29 lengo likiwa kutabanaisha mchango mkubwa unaofanywa na walinda amani kote duniani katika jamii mbalimbali zinazopitia changamoto huku mwaka huu maudhui yakiwa amani, watu na maendeleo.
Walinda amani Tanzania kurekebisha barabara
Leave a comment