NA MWANDISHI WETU, GEITA
WATU wasiojulikana wamevamia na kupora fedha kwenye maduka 14 yanayotoa huduma ya kifedha katika Kitongoji cha Kilimahewa, Kata ya Ludete Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro wilayani Geita.
Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa kuamkia Jumanne Mei 23, mwaka huu saa saba usiku ambapo watu hao wakiwa na silaha za moto walivamia maduka na kupora.
Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo, Patrick Bilago alisema alipata taarifa za uhalifu huo saa 10:30 alfajiri na kukuta milango ya duka imevunjwa.
“Kulikuwa na Sh milioni mbili na laki sita zote wamechukua, yaani kila kitu wamevunja, kila kitu wameharibu kila kitu kwenye ofisi yangu na kwenye ofisi za majirani zangu,” alisema Bilago na kuongeza:
“Ni tukio ambalo limeturudisha nyuma sana kimaendeleo, wahusika hatukuweza kuwafahamu kwa kuwa tukio limetokea usiku, hatukuweza kuwatambua moja kwa moja kwa hiyo serikali ipo itatusaidia.
”Naye Philipo Stanslaus alisema taarifa za tukio zimetolewa na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Katoro na kueleza wezi hao wamefanya uhalifu mkubwa japokuwa eneo hilo lilikuwa na walinzi wanaolipwa. “Kila siku walinzi wanakuwepo mpaka tunafunga, hatujui nini kimetokea labda walizidiwa, kwa hiyo tunaiachia serikali kwa uchunguzi zaidi. Dukani kwangu kulikuwa na simu pamoja na pesa.
”Katibu wa soko hilo, Jonathan Bernard alieleza kuwa baada ya kupokea taarifa za tukio hilo, walifanya juhudi za kuliarifu Jeshi la Polisi ambao waliwasili eneo hilo na kuanza kufanya uchunguzi wa tukio.
“Maduka yaliyovamiwa ni ya huduma za kifedha ikiwemo Tigo Pesa, M-Pesa na huduma za kibenki, wamevamia, wamevunja na kupora pesa zilizokuwemo kwenye hayo maduka, haijafahamika kiasi.”
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza mpaka jana asubuhi hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa ambapo Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka wahusika.
“Jambo hili halikubaliki hata kidogo, na ni jambo ambalo linapaswa kupigwa vita na kukemewa kabisa katika jamii yetu na wilaya yetu, nitoe wito kwa wananchi kila mmoja awe mlinzi wa mali zake. “Lakini sisi kama serikali tunaendelea kutimiza wajibu wetu, kupitia jeshi letu la polisi, kuhakikisha kwamba usalama wa watu na mali zao unaimarika,” alisema Magembe