NA MWANDISHI WETU, SHINYANGA
WAKALA wa vipimo nchini (WMA) mkoani Shinyanga wamewashauri wafanyabiashara kuweka nembo kwenye vifungashio, ili kutambulika kisheria kwa usalama wao na bidhaa zao.
Hayo yamesemwa leo Mei 20, 2023 na Kaimu Ofisa Vipimo Mkoa, Happiness Saronge, wakati akizungumza na wafanyabiashara wa mchele eneo la Ibinzamata Manispaa ya Shinyanga kuadhimisha Siku ya Vipimo duniani, yenye kauli vipimo vinavyotumika kwenye mfumo wa chakula duniani.
Saronge amesema wanatoa elimu ya vifungashio, wafanyabiashara wanatakiwa wawe na nembo, ili ijulikane imetengenezwa lini, muda wa kuisha matumizi yake na vipimo vilivyomo kama ni sahihi.
“Wafanyabiashara kila mwaka wanatakiwa kukaguliwa mizani zao, lengo ni kuona kama inapunja mteja au kujipunja na wenye mizani mipya wahakikishe inakaguliwa, wapo wanaofanya udanganyifu katika kufungasha,”amesema Saronge.
Amewataka wanaofungasha waweke pia majina yao kwa kutumia mashine sio kwa kuandika na kalamu, hilo ni kosa kisheria.
Amesema marekebisho ya mzani yanafanyika kwa gharama kidogo kwa kutofautisha aina ya mizani aliyonayo mfanyabiashara.
Baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria utolewaji wa elimu hiyo, akiwemo Joel Albert, amesema wakulima vijijini wao wenyewe wanapenda kutumia vipimo vya ndoo, wakienda na mizani wanaikataa kwa kudai hawaiamini.
Ezekiel Mabala amesema wao ni wafanyabiashara wanaouza kwa rejareja, kuweka nembo itakuwa ni ngumu, kwa sababu hawatumii vifungashio, mteja anakuja moja kwa moja mashine kuchukua mchele akiwa na kifungashio chake.
Wafanyabiashara hao waliomba Wakala wa vipimo inapofika wakati wa ukaguzi mizani waende moja kwa moja kwenye maeneo yao, siyo kwenye ofisi za watendaji wa kata unakuwa ni usumbufu.