NA SALOME MAJALIWA, JKCI, KISARAWE
WANANCHI wa Kisarawe na wilaya jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za upimaji, ushauri na matibabu ya moyo zinatotolewa na watalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya wilaya Kisarawe.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Fatma Nyangasa wakati akifungua kambi maalumu ya siku tatu ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanyika katika Hospitali ya wilaya Kisarawe.
Amesema kuwepo kwa kambi hiyo ya matibabu kunatekeleza azma ya Rais wa awamu ya sita Dk. Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo.
“Wananchi wa Kisarawe mjitokeze kwa wingi kuchuguza afya zenu endapo mtagundulika kuwa na maradhi ya moyo mtapatiwa tiba hapa hapa Kisarawe kwani tumejipanga kuwahudumia na hii siyo kwa Kisarawe peke yake bali na maeneo ya jirani”.
“Kwa kushirikiana na wenzetu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tumesogeza huduma kwa wananchi wetu wa Kisarawe kwa kufanya upimaji na matibabu ya moyo. Wataalamu hawa wapo hapa kwaajili ya kutoa huduma hii,na huu ni mwendelezo wa kupatikana kwa huduma nyingine za kibigwa katika hospitali hii ya wilaya kwani vifaa tiba vipo, dawa zipo za kutosha, wataalamu wapo uko tayari kuwahudumia wananchi wote”,amesema DC Nyangassa
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Baraka Ndelwa alisema wapo Kisarawe kwaajili ya kutoa huduma za kibingwa za upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wote wa Kisarawe pamoja na wilaya jirani.
Dk Ndelwa amesema licha ya kutoa huduma ya upimaji na matibabu ya moyo wanatoa pia elimu kwa wananchi ya kujikinga na magojwa hayo na jinsi ya kutumia dawa kwa usahihi kwa wale ambao ni wagonjwa wa moyo.
“Tumekuja katika hospitali ya wilaya ya Kisarawe kwaajili ya kutoa huduma bobezi kwa wananchi na kuwapa elimu ya mtindo bora wa maisha ili wajikinge na maradhi ya moyo kwani maradhi haya yanazidi kuongezeka kwa sababu jamii haina elimu ya kutosha ya jinsi ya kujikinga na maradhi ya moyo”,alisema Dk.Ndelwa.
Naye Mganga Mkuu wa Kisarawe Dk Zaituni Hamza amesema hiyo ni kambi ya kwanza ya matibabu ya magojwa ya moyo kufanyika katika hospitali ya wilaya na wanategemea kuwahudumia wananchi wote wa Kisarawe na maeneo ya jirani.
Ameema wataalamu hao watatoa huduma za kimatibabu pamoja na uchunguzi wa kina wa moyo kwa kutumia machine ya kuuchunguza moyo namna unavyofanya kazi (Echocardiograph).
Akizungumzia uwepo wa kliniki ya magonjwa ya moyo Dk.Hamza amesema mara baada ya kumalizika kwa kambi hiyo madaktari wa magonjwa ya moyo wa (JKCI) wataendelea kuwaona wagonjwa wa moyo katika hospitali ya Kisarawe.
“Kumalizika kwa kambi hii ya matibabu sio mwisho wa kutolewa kwa huduma hizi za magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Kisarawe,huduma hii itaendelea kutolewa na madaktari wa (JKCI) kwa wananchi kwa utaratibu tutakaouweka”.
Wananchi waliopata huduma ya uchunguzi na matibabu katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kuiomba Serikali iwe inaitoa mara kwa mara kwani inawasaidia kupata huduma kwa urahisi zaidi tofauti na kama wangeifuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam.
Ahmad Nguyu mkazi wa Kilombero mkoani Morogoro amesema katika kambi hiyo amepata huduma nzuri ya uchunguzi, ushauri na kupewa dawa za kutosha za kwenda kutumia.
‘’Baada ya kufanyiwa uchunguzi nimegundulika nina tatizo la shinikizo la juu la damu nimepewa dawa za kutumia,nashukuru kwa huduma niliyoipata ninaomba huduma hii iendelee kutolewa na sehemu nyingine ili wananchi wote waweze kufaidika nayo”, .ameeleza Nguyu