NA MWANDISHI WETU, TANGA
KAMATI za Ujenzi za utekelezaji wa Mradi wa Boost mkoani Tanga zimesisitizwa kufuatilia kwa ukaribu hasa matumizi ya vifaa vinavyotumika katika ujenzi.
Akifungua semina iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Tanga (TAKUKURU) Mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa amewataka Madiwani, Watendaji, Walimu na Kamati ya ujenzi ya utekelezaji wa Mradi wa BOOST kuhakikisha Mradi huon unakamilika kwa wakati na ubora kama ilivyoelekezwa na Serikali.
” Tumekusanyika hapa lengo ni kuwajengea uwezo wa kusimamia miradi hiyo kwa uaminifu na kuepukana na vitendo vya rushwa” amesisitiza Mgandilwa.
Aidha amewataka Watendaji hao kusimamia mradi huo kwa kushirikisha jamii katika utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kufahamu kinachoendelea.
” Leo tumepata ushiriki wa Waheshimiwa Madiwani si vibaya fedha tunazozipata kutoka Serikali Kuu tukaenda kuieleza jamii na nyaraka ambazo tunapewa za wazi tukatengeneza mbao za matangazo kuonesha kiasi cha fedha tulizopata na utekelezaji wake huo ndio sehemu ya uwazi wa utekelezaji wa miradi ya Serikali” alieleza Mgandilwa.
Awali Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga Victor Swella amesema semina hiyo inafanyika Mkoa mzima ikiwa ni maelekezo waliyopewa na kusimamia fedha za Mradi wa BOOST.
“Kamati zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo ziweze kusimama katika nafasi yake kwa mujibu wa kanuni sheria na maadili yote ya usimamizi.”
Naye Mratibu wa Mradi wa BOOST Mkoa wa Tanga Onesmo Simime kutoka Idara ya Elimu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, amesema Mkoa huo umepokea zaidi ya Sh.Bilioni 11 kwa ajili ya utekelezaji.
“Ni muhimu Watendaji kuwa makini kwa kusimamia miradi hiyo kwa uangalifu na kuhakikisha unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa” alihitimisha Simime




