NA MWANDISHI WETU
Klabu ya soka ya Yanga ya Tanzania itakutana na USM Alger ya Algeria kwenye fainali ya kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF).
Yanga imetinga fainali jana Jumatano, Mei 17 baada ya kuifurusha timu ya Marumo Gallants ya Afrika kusini kwa magoli 2-1.
Ikumbukwe klabu hizo kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam, Tanzania, Yanga ilishinda magoli 2-0.
Kwa upande wake, USM Alger imetinga fainali baada ya kuifungashia virago timu ya Asec Mimosas ya Ivory Cost kwa magoli 2-0 jana Jumatano.
Mechi ya kwanza kati ya Mimosas na USM Alger ilimalizika 0-0 lakini jana wababe hao wa Algeria walio katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ya nyumbani kwao, walifanikiwa kuutumia vema uwanja wa nyumbani.
Hii ni mara ya kwanza kwa klabu ya Yanga kufika nusu fainali tangu ianzishwe mwaka 1935 na kubwa zaidi klabu hiyo sasa imefika fainali.
Tayari wadau wa soka mbalimbali wanaipa nafasi kubwa Yanga kutwaa kombe hilo wakisema wababe hao wa Jangwani wana morali ya juu ya kutaka kufanya maajabu.