NA ANDREW CHALE,DAR ES SALAAM
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa Elimu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini juu ya usajili wa Makampuni na Majina ya Biashara katika semina iliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), cha jijini Dar es Salaam.
Awali akiwasilisha mada katika semina hiyo, Ofisa Usajili kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Greyson Mushi ametoa mada juu ya umuhimu wa urasimishaji wa biashara na Kampuni kwa Kufuata taratibu maalumu za kufungua ambazo pua zinapatikana kwenye mfumo wa Brela.
Aidha, Mushi alizitaja aina tatu za kampuni zinazosajiliwa BRELA kuwa ni Kampuni za nje (Foreign Company), Kampuni binafsi (Private Company), na Kampuni za Umma (Public Company).
“Taratibu za usajili wa kampuni ambao unafanyika kwa njia ya mtandao wa (ORS) unaopatikana katika tovuti ya BRELA www.brela.go.tz ni rahisi kwa kila mtu kutumia.
Hatua bora na nzuri kwani umerahisisha utoaji wa huduma.” amesema Mushi
Semina hiyo imehudhuriwa na wadau wa uwekezaji kutoka vyuo vikuu, Watu binafsi wenye makampuni na wanafunzi wa Vyuo vya Chuo kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), na Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Uwekezaji na Wajasiriamali nchini, Sebastian Kingu amewasisitiza vijana kutumia fursa ya kujiunga katika umoja ili kufungua kampuni zao binafsi zitakazo wawezesha kujikwamua kiuchumi na kuendana na kasi ya mabadiliko ya Sayansi na teknolojia.
Semina hiyo iliyofanyika katika chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), cha Jijini Dar es Salaam iliandaliwa na Umoja wa Uwekezaji na Wajasiriamali nchini Tanzania Pan African Investors Association (TAPAIA), ilihusu fursa za Vijana kujiunga na kufungua kampuni binafsi ili kujikwamua na changamoto za ajira nchini sambamba na kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia