NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam CPA, Amos Makalla amemtaka Mkandarasi wa kampuni ya Serengeti anaetekeleza Mradi wa Visima vya Maji Kimbiji na Mpela kurudi site mara Moja baada ya mkandarasi huyo kusuasua na kuingia mitini.
CPA, Makalla ametoa maelekezo hayo leo Mei 9, 2023 wakati wa Ziara ya kukagua kama mradi huo unaendelea au umesimama na kuthibitisha pasipokuwa na shaka kuwa Kazi zimesimama kwa muda mrefu.
Kutokana na hilo, CPA Makalla amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Halima Bulembo kuweka kambi kwenye Miradi hiyo na kuhakikisha kazi usafishaji wa Visima inafanyikwa kwa Kasi Ili vikamilike mapema.
Aidha CPA, Makalla ametoa muda wa wiki Moja kwa Bodi na Menejimenti ya DAWASA kumkabidhi mpangokazi wa ujenzi wa miundombinu ya kupokea Maji kutoka kwenye visima hivyo na kuyapeleka kwenye bomba Kuu.