NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza ujenzi wa Barabara za ndani kwa lengo la kurahisisha usafirishaji na kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdullah ametoa kauli hiyo mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa wakati akiwasalimia waumini wa Masjid Khadija Bint Khuwaylid Kikungwi Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema Serikali inatambua na kuthamini shughuli zinazofanywa na wananchi wa kikungwi katika kupambana na kupunguza umaskini hasa kujielekeza katika Sekta ya Uchumi wa Buluu ambapo Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha barabara hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa mbali na changamoto hiyo ya Barabara Serikali itaendelea kuzishughulikia changamoto mbali mbali zinazokikabili kijiji cha kikungwi ikiwemo Umeme kuwa mdogo, ukarabati wa madarasa ya msingi pamoja na huduma ya maji safi na salama ili wananchi wafurahie upatikanaji wa huduma hizo.
Hemed ameitaka Serikali ya Mkoa wa Kusini Unguja kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mipango ili wananchi hao waondokane na changamoto hizo.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwasisitiza wananchi kuendelea kuitunza amani na utulivu iliopo nchini na kueleza kuwa Tanzania inasifika kwa uwepo wa amani na utulivu hatua ambayo inatoa fursa kwa Wawekezaji kuja kuwekeza pamoja na kuongezeka kwa Idadi kubwa ya Watalii wanaoingia nchini.
Aidha Hemed aliwakumbusha waumini hao kusimamia maadili mema kwa vijana wao na kuendelea kupiga vita matendo maovu yanayoibuka ndani ya jamii.
Naye Maalim Vuai Rajab amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa uamuzi wake ya kujumuika na waumini hao katika Ibada ya Sala ya Ijumaa hatua ambayo inaonesha Imani ya viongozi wakuu kuwa karibu na wananchi wao.
Aidha aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwasogezea Umeme kijijini hapo na kueleza kuwa bado umeme ni mdogo hivyo wameomba kutatuliwa tatizo hilo ili kuwasaidia katika shughuli zao mbali mbali za kiuchumi.