NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema bei ya mafuta ya kupikia imeshuka.
Dk Kijaji aliyasema hayo bungeni Dodoma jana wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2023/24.
Alisema kushuka kwa bei kunatokana na kuondolewa kwa vikwazo vya biashara kwa baadhi ya nchi zinazozalisha na kusambaza kwa wingi mafuta ya kupikia katika soko la dunia.
Dk Kijaji alisema kati ya Julai mwaka jana na Machi mwaka huu wastani wa bei ya mafuta ya alizeti imeshuka kutoka dola za Marekani 1,491.30 kwa tani moja kwa kipindi cha Machi mwaka jana hadi dola za Marekani 1,088.10 sawa na upungufu asilimia 27.03.
Alisema pia bei ya mafuta asili ya mawese imeshuka kutoka dola za Marekani 1,776.96 kwa tani moja kwa kipindi cha Machi mwaka jana hadi kufikia dola za Marekani 975.63 kwa kipindi cha Machi mwaka huu sawa na upungufu wa asilimia 45.09.
Aidha, Dk Kijaji alisema mwenendo wa bei za vifaa vya ujenzi kwa mwaka 2022/23 umeendelea kushuka na kuonesha uhimilivu hasa kwa upande wa nondo.
Alisema wastani wa bei ya nondo moja ya mm 12 imeshuka kutoka Sh 26,865 kipindi cha Februari mwaka jana hadi Sh 24,417 Februari mwaka huu sawa na upungufu wa asilimia 9.1.
Dk Kijaji alisema nondo moja ya mm 16 imeshuka kutoka Sh 46,097 hadi Sh 45,587 sawa na upungufu wa asilimia 1.1, nondo moja ya mm 10 imeshuka kutoka Sh 19,450 hadi Sh 18,629 sawa na upungufu wa asilimia 4.2.
Alisema pia bei ya nondo moja ya mm 8 imeshuka kutoka Sh 15,250 hadi Sh 15,083 sawa na upungufu wa asilimia 1.1.
Dk Kijaji alisema pia wastani wa bei ya saruji imeonesha uhimilivu kwa kuwa mfuko mmoja wa kg 50 ulikuwa Sh 17,606 Februari mwaka jana na Sh 17,688 Februari mwaka huu.
Aliwaeleza wabunge kuwa bei ya mabati imeongezeka kwa asilimia 6.4 kutoka shilingi 23,091 kwa kipindi cha Februari mwaka jana hadi Sh 24,563 Februari mwaka huu mtawalia.
Aidha, Dk Kijaji alisema pia kumekuwa na ongezeko la bei za mazao ya chakula nchini.
“Wastani wa bei ya maharage imepanda kutoka Sh 215,193 kwa gunia la kilo 100 mwezi Februari, 2022 hadi kufikia Sh 301,297 mwezi Februari, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 40,” alisema.
Alisema wastani wa bei ya mahindi kwa gunia la kilo 100 imeongezeka kutoka Sh 90,330 Februari mwaka jana hadi kufikia Sh 115,141 Februari mwaka huu sawa na ongezeko la asilimia 27.5.
Pia wastani wa bei ya mchele kwa gunia la kilo 100 imeongezeka kutoka Sh 216,738 Februari, 2022 hadi Sh 291,819 Februari, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 34.6.