NA MWANDISHI WETU, DODOMA
SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema hana hofu na mbunge wa zamani wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi’ Sugu’ endapo watakutana katika mchakato wa uchaguzi mkuu utakaokuwa huru na haki.
Dk Tulia ametoa msimamo huo leo Mei 4, 2023 wakati akijibu swali katika mahojiano maalumu na runinga moja nchini na kufanyika katika makazi rasmi ya Spika Jijini Dodoma.
Pamoja na mambo mengine, Spika aliulizwa ikiwa hatishiki kukabiliana na Sugu’ katika uchaguzi unaoitwa huru na haki, hasa ikizingatiwa kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, wapinzani wengi waliamini kuna nguvu ya ziada ya dola ilitumika kuwabeba walioshinda.
“Sihofii kupambana naye, niko vizuri sina wasiwasi na hilo naomba Mungu aniweke, nimefanya kazi kubwa, nyie nendeni Mbeya Mjini mtaamini,’ amejinasibu Dk Tulia.
Na akaongeza kusema: “Hata yeye anajua (Sugu), hao wanaojadili mtandaoni nadhani hawajafika Mbeya wala hawapajui wala kuwasikia Mbeya, sasa nyie (waandishi) mnakaribishwa halafu mtawanyike na mkaulize hapa Mbeya Mjini mbunge ni nani, mtapata majibu.”
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 uliolalamikiwa na vyama vya upinzani, Dk Tulia alishinda kwa kura 75,225 dhidi ya Sugu aliyepata kura 37,591 licha ya kuwa aliliongoza jimbo hilo kwa miaka 10 mfululizo kuanzia mwaka 2010/20.
Dk Tulia amejivunia mafanikio yanayotokana na kazi alizozifanya kwa kusema kuwa wakati wa kampeni ahadi zilikuwa nyingi zikiwemo za Mbunge na Ilani ya CCM.
Kati ya ahadi hizo kwa mujibu wa Spika Tulia, ilikuwa ni kujenga barabara ya njia nne kuanzia Igawa hadi Tunduma kwa kilomita 218, ambapo ameomba wameomba awamu ya kwanza ya ujenzi ianzie Mbeya Mjini ili kupunguza changamoto ya foleni.
“Hivi sasa Serikali imeshaingia mkataba na mkandarasi ameshaanza majukumu yake. Jambo jingine ni mradi wa maji Mbeya kuna watu wengi wanaongezeka kwa nyakati tofauti, bado kuna changamoto ya maji baadhi ya maeneo,” amesema.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo, aliwaahidi wapiga kura wake kumaliza changamoto hiyo akisema: “Tuliwaahidi kumaliza changamoto hiyo na kwa sasa mkandarasi yupo eneo la kazi kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa Mto Kiwila utakaoleta maji Mbeya mjini,”amesema Dk Tulia.
Kukamalika kwa ahadi hizi pamoja na mengine mengi, kunamfanya Spika Tulia kama ndiyo vigezo vitakavyo washawishi wana Mbeya kumpigia kura nyingi ili aendelee kuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa kipindi kingine cha miaka mitano.