NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani limezifuta leseni 3,214 za madaraja C na E za madereva waliokuwa wakiendesha malori na mabasi ya abiria.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’anzi amesema Dar es Salaam jana kuwa leseni zilizofutwa ni kati ya leseni 20,940 zilizohakikiwa hadi Aprili 30, mwaka huu.
Kamanda Ng’anzi amesema kuwa madereva waliokuwa wakimiliki leseni hizo hawana sifa ikiwamo ya kusomea madaraja hayo.
Amesema leseni zilizofutwa zilionekana kutokidhi vigezo kwa sababu wahusika wamezipata visivyo halali na wameshushwa madaraja hadi ya awali ambayo ni D na B.
Kamanda Ng’anzi amesema leseni 17,726 zilibainika kuwa zimekidhi vigezo na hadi sasa wamehakiki asilimia mbili ya leseni za madereva wa madaraja C na E.
Amesema uhakiki awamu ya kwanza ulianza Machi Mosi kwa hiari kwa madereva kutakiwa kufika ofisi za wakuu wa usalama barabarani kuhakiki leseni zao na kazi hiyo ilipangwa kukamilika Aprili 30, mwaka huu.
Kamanda Ng’anzi amebainisha kuwa wameongeza muda hadi Julai 31, mwaka huu ili kutoa nafasi kwa madereva kusomea madaraja E na C kwa sababu kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu za jeshi, ni lazima dereva apite katika shule za udereva.
“Niliwaambia wakuu wa usalama barabarani madereva wasibuguziwe tuwaache wenyewe waje kwa hiyari ila tukianza kuwapekuwa na kuwakamata tutawauliza na kuwahoji katika kipindi hiki tulichokuwa tumetoa muda wa kuhakiki wa hiyari walikuwa wapi kuhakiki,” ameeleza Kamanda Ng’anzi.
Mwishoni mwa Februari mwaka huu, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali Camilius Wambura alilifuta Dawati la Leseni la Jeshi la Polisi baada ya kubaini kuna ukiukwaji wa maadili.
Baada ya uamuzi huo, liliundwa dawati jipya la utoaji wa leseni na kikosi kilitakiwa kuhakiki ni leseni zipi zilipatikana kiuhalali na zipi hazikufuata utaratibu na kujua dereva gani ni mahiri katika eneo lake la udereva.