NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeruhusu mabasi ya mikoani yaanze safari saa tisa usiku.
Latra imeagiza wamiliki wa mabasi wanaopenda kuanza safari muda huo wafike katika ofisi za mamlaka hiyo kuomba leseni na masharti ni lazma madereva wasajiliwe ili kuwa na taarifa zao.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Priscus Joseph alisema hayo Dar es Salaam akiwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Latra, Salum Pazzy.
Pazzy aliwaleza waandishi wa habari kuwa Latra inafanya kazi kwa kushirikisha wadau wakiwamo Taboa na hawana mvutano kuhusu muda wa kuanza safari za mabasi kwenda mikoani.
“Tunafanya kazi kwa kushirikiana, suala la kubadilisha ratiba za mabasi awali muda ulikuwa ni mabasi yote lazima yaanze safari saa 12 asubuhi si zaidi ya hapo, lakini baadaye tuliruhusu ratiba zianze saa 11 asubuhi,” alisema.
Pazzy alisema utaratibu huo wa majaribio wa kuanza safari saa 11 alfajiri ulianza Novemba mwaka jana na hadi sasa mabasi 180 yamepewa leseni kuanza safari muda huo na kuwa hivi karibuni wamepokea ushauri kutoka bungeni wa kutaka mabasi hayo yafanye safari saa 24.
“Safari hizi za kuanzia saa 11 ni kwa majaribio na juzi bungeni wametoa ushauri wa kutaka safari zifanywe saa 24, tumepanua wigo kwa kuwashirikisha wadau wakiwemo Taboa na ratiba sasa inaanza saa tisa alfajiri na tumesema wanaotaka waje na masharti ni lazima madereva wa mabasi hayo wasajiliwe Latra ili tujue nani yuko na gari hilo muda huo,” alisema.
Katibu Mkuu wa Taboa, Joseph alisema wanafanya kazi kwa ushirikiano na Latra na hawana mvutano.
“Hatuna mvutano, tulishauri tuanze safari saa 24, hivyo tunaomba vyombo vya serikali vyote kama Jeshi la Polisi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) watusaidie ili kufanikisha azma hiyo,” alisema Joseph na kuongeza:
“Usalama tunaoomba ni ule wa polisi wa kudhibiti wizi, ujambazi, Tamisemi tunaomba zile huduma zinazotolewa kwenye vituo vya mabasi zitolewe saa 24 kwa mfano bodaboda zinazoleta abiria waruhusiwe kufika kituoni muda wowote hata usiku, pia vyombo vya usafiri vile vya ndani ya mkoa navyo viruhusiwe kuleta abiria muda wowote.”
Pazzy alisema hivi sasa wanaendelea kuboresha kanuni za usafiri na usafirishaji na kuanzia Mei 15 hadi 19 kutakuwa na mikutano ya wadau kutoa maoni ya kuziboresha.