NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WATU wawili wanahofiwa kufariki dunia, baada ya bajaji waliyokuwa wamepanda kugogwa na eneo la Mabibo Gereji.
Ajali hiyo imetokea leo Jumatano Mei 3, 2023 saa moja asububuhi wakati bajaji hiyo ikitokea Buguruni kuelekea Ubungo kukatiza upande wa pili bila kuchukua tahadhari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Mtatiro Kitinkwi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, na kueleza kuwa atatoa taarifa kamili baadaye baada ya kupokea taarifa kutoka kwa madaktari.
“Ni kweli kuna taarifa ya hivyo, watu watatu wameondolewa pale wakiwa na hali mbaya na kukimbizwa hospitali, timu ya madaktari na askari wetu wanaendelea tutapata mrejesho kama wamefariki au wapo hai,”amesema Kamanda Kitinkwi.
Amesema ajali hiyo imehusisha watu watatu waliokuwepo kwenye bajaji, ambao ni wanaume wawili na mwanamke mmoja.
“Hapa tunasubiri madaktari watuambie au watuandikie kuthibitisha, ila wamekimbizwa hospitali ya Mwananyamala wakiwa na hali mbaya, chanzo cha ajali ni dereva wa bajaji kuhamia upande wa pili bila kuchukua tahadhari,”amesema.
Mohamed Shaban ambaye ni shuhuda wa ajali hiyo amesema, gari ndogo ilikuwa ikitokea Ubungo kuelekea Buguruni na dereva wa bajaji alikuwa akitoka Buguruni kuelekea Temeke.
“Tulikuwa tumekaa hapa ghafla tukasikia kishindo kama cha bomu, kuangalia tukaona bajaji imerushwa kule huku watu wawili wakiwa wamelala hawajitambui na mmoja akijitahidi kuomba msaada,”amesema Shaban.
Shuhuda mwingine Alex Leonard ameeleza kuwa wakati anatokea upande wa Buguruni alikuwa ameongozana na bajaji hiyo yeye akiwa kwenye bodaboda, akaingia kituo cha mafuta kuweka mafuta alipoondoka ndipo akakuta ajali hiyo imeshatokea.
Amesema madereva wa bajaji wamekuwa na mtindo wakifiki eneo hilo, huvuka upande wa pili na kuingia hifadhi ya barabara ili kukwepa askari waliopo eneo la External.
“Ukiangalia mazingira ya ajali inaonesha dereva wa bajaji alivuka bila kuangalia upande mwingine hakuchukua tahadhari, hivyo ajali hii imechangiwa na uzembe,”amesisitiza Leonard.