NA FARIDA RAMADHANI, WFM, DODOMA
Serikali imewalipa wateja wa iliyokuwa Benki ya FBME jumla ya shilingi bilioni 2.43 ikiwa ni malipo ya awali ya fidia ya bima ya amana kwa wateja 3,446, hadi mwezi Machi, 2023.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Chande alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chwaka, Makame Haji, aliyetaka kujua ni lini Serikali itawalipa waathirika wa Benki ya FBME iliyofilisiwa tangu Mei 2017.
Chande amesema kuwa malipo hayo yamefanyika kupitia Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kwa wateja wa Benki hiyo waliojitokeza kuidai malipo hayo.
“Malipo ya fedha za ufilisi (liquidation proceeds) kwa wateja wenye amana zaidi ya shilingi milioni 1.5 yanayotokana na uuzaji wa mali, makusanyo ya madeni, mikopo na fedha nyingine za Benki hiyo yatafanyika ndani ya mwaka huu wa fedha 2022/23”, amesema Chande.
Ameongeza kuwa fedha za ufilisi zitalipwa baada ya Mahakama ya Cyprus kutoa uamuzi kuhusu pingamizi lililowekwa na Benki Kuu ya Cyprus la kuitambua DIB kama Mfilisi wa benki yote ikijumuisha makao makuu pamoja na tawi la Cyprus (Global liquidator), uamuzi unatarajiwa kutolewa ndani ya mwaka wa fedha 2022/23.