NA MWANDISHI WETU
KIKOSI cha Sita cha Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania (TANBAT6) kinacholinda amani Afrika ya kati kimetakiwa kuendeleza umoja hasa wakati wote wanapotekeleza majukumu mbalimbali ya kulinda amani nchini humo.
Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Mwambata wa Jeshi la Tanzania anayehudumu kazi yake Jamhuri ya Afrika ya kati Brigedia Jenerali Absolomon Shausi wakati alipofanya ziara ya kutembelea kikosi hicho cha TANBAT6 wanaohudumu chini ya Ujumbe wa Kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati Kanda ya Magharibi (MINUSCA).
Akizungumza na maofisa hao ambao walianza kwa kumkaribisha kwa kuimba nyimbo za morali, Brigedia Jenerali Shausi alisema ni muhimu kwa walinda amani kuendeleza umoja na mshikamano katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema ameshuhudia walinda amani wa Tanzania walivyojipanga na kwamba nivigumu kutofautisha kwamba huyu ni watanzania na huyu ni wa Nepal, kwani wanatekeleza majukumu yao kwa ushirikiano kama vile wametoka kwenye jeshi moja.
“Nasifu pia utimamu wa jeshi la Tanzania, umahiri ambao mnaendelea kuuonyesha unadhihirisha dhahiri kuwa mnakiwango kikubwa cha nidhamu na mmejifunza vema kutekeleza majukumu yenu,” amesema Brigedia Jenerali Shausi.
Akitoa shukurani zake kwa niaba ya kikosi cha TANBAT6, Luteni Kanali Amini Mshana amesema kuwa wamempokea kwa furaha mwambata huyo wa jeshi aliyekuja kujitambulisha kwao lakini pia kuona utimamu na utayari wa kikosi hicho kilichopo chini ya MINUSCA.
Luteni Kanali Mshana amesema yeye na wanakikosi wenzake wanaahidi kudumisha yote waliyoelekezwa katika utendaji wa ulinzi wa amani nchini Afrika ya kati.