NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Maboresho ya Baraza la Kiislamu Tanzania (Bakwata) Sheikh Issa Issa na wajumbe wake wanne kuandika barua ya kujivua nyadhifa zao, leo Mei mosi 2023, Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar bin Zubeir ameridhia ombi hilo.
Kuridhiwa kwa ombi hilo, kumempa nafasi Mufti huyo kumteua Kamishna mstaafu wa Polisi, Alhaj Suleiman Kova kuwa mwenyekiti wa Tume hiyo ya Bakwata.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Mufti wajumbe wengine wa tume watatangazwa hivi karibuni baada ya kukamilika kwa mchakato wa uteuzi.
Aprili 30, 2023 mwenyekiti huyo na wajumbe wake waliomba ridhaa kuachia madaraka yao kupitia barua waliyoielekeza kwa Mufti wakieleza wameshindwa kutekeleza majukumu waliyopatiwa kutokana na ugumu wanaoupitia.
Miongoni mwa majukumu waliyoelekezwa ni kufanya uchunguzi wa mali za Bakwata zinazomilikiwa kinyume na utaratibu na kuchukua hatua za kutatua.
Pia kufanya tathmini ya changamoto za mifumo ya utawala inayoikabili Bakwata na kushauri namna ya kufanya maboresho pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa Bakwata.
Mmoja wa wajumbe hao walisema majukumu hayo pamoja na mengine wameshindwa kuyatekeleza kutokana na kutopata ushirikiano.
Wajumbe wa tume hiyo iliyozinduliwa Februari mwaka huu ni Sheikh Mohammed Nyegi, Daudi Nasib, Idi Kamazima pamoja na Omar Ege.